KIGOMA; WADAU wa uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wametakiwa kutumia taratibu zinazoakisi 4R za Rais Samia Suluhu Hassan, ili kuwezesha uchaguzi wa serikali za mitaa katika halmashauri hiyo kuwa huru, wa haki na shirikishi.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dk. Semistatus Mashimba ametoa maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wilayani katika mkutano uliohusisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wazee maarufu, vyama vya wafugaji na wakulima, watendaji wa vijiji na kata pamoja na waandishi wa habari.
Dk Mashimba ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, amesema ni takwa la kisheria linalomtaka kufanya hivyo, ili wananchi wapate maelezo siku 62 kabla ya tarehe ya uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa wapiga kura pamoja na wagombea kupata taarifa zote kwa wakati na kwamba 4R za Rais Samia ndiyo nafasi yake kufanyiwa kazi kikamilifu.
Soma pia: Samia asisitiza haki uchaguzi wa serikali za mitaa
Amesema kuwa kampeni katika uchaguzi huo zitaanza Novemba 20-26 na uchaguzi utafanyika Novemba 27 mwaka huu na kuomba viongozi wa vyama vya siasa, dini na wadau wote kwenye halmashauri hiyo kudumisha amani na utulivu, ili kuwezesha uchaguzi kufanyika bila changamoto yeyote.