Wadau watakiwa kubuni mifumo jumuishi kifedha fursa dhahabu

DAR ES SALAAM: WADAU wa sekta ya madini nchini wametakiwa kubuni na kutekeleza mifumo jumuishi ya kifedha itakayowezesha kufungua fursa za sekta ya dhahabu.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Yamungu Kayandabila ameyasema hayo Dar es Salaam wakati wa kufungwa kwa kongamano la wadau wa sekta ya umma na binafsi lililoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Biashara Afrika (Afreximbank) kwa kushirikiana na BoT.

“Ingawa sekta ya madini ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wetu inashika namba mbili baada ya utalii lakini bado haijafikia uwezo wake kamili. Ni wakati sasa kwa wadau kuja na suluhisho la kweli kama vile kubuni mifumo ya kifedha inayolenga maendeleo ya sekta hii,” amesema Kayandabila.

Amesema wachimbaji wadogo na wa kati wengi wamejikita katika uchimbaji wa namna isiyo rasmi, jambo linalokwamisha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha kutokana na ukosefu wa kumbukumbu sahihi za kifedha pamoja na hatari kubwa za uendeshaji.

Kongamano hilo lenye kaulimbiu: ‘Suluhisho Bunifu za Ufadhili kwa Ukuaji Endelevu wa Tanzania’ iliwakutanisha wadau wa sekta ya madini, fedha na sera ili kujadili fursa za kiuchumi na mikakati ya ushirikiano.

Mkurugenzi Mkuu wa Mahusiano na Wateja wa Afreximbank, Eric Intong, amesema benki hiyo imejikita kusaidia ukuaji jumuishi wa sekta ya madini, hasa kwa wachimbaji wadogo.

“Sekta ya madini ni muhimu si tu kwa Tanzania, bali kwa bara zima, bado ukuaji wake unakwamishwa na changamoto za kimuundo na kifedha,” amesema Intong.

Amesema Afreximbank inaelekeza msaada kupitia mikakati miwili mikuu: kwanza, kutoa fedha za moja kwa moja kusaidia wachimbaji wadogo kupata vifaa vya kisasa, na pili, kujenga uwezo wa ndani sambamba na sera za taifa za ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta hiyo.

Aidha, benki hiyo imerudia tena kauli yake ya kutangaza kutoa ufadhili wa Dola za Marekani bilioni moja (Sh trilioni 2.6) katika kipindi cha mwaka ujao ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuibadilisha sekta ya madini na sekta nyingine hususan miradi ya kimkakati kuwa kichocheo jumuishi na chenye tija zaidi kwa uchumi wa nchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button