Wafanyabiashara 42 wa Comoro kushiriki Sabasaba

DAR ES SALAAM – WAFANYABIASHARA 42 kutoka nchini Comoro wanatarajiwa kushiriki maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu imeeleza kuwa ushiriki wa wafanyabiashara hao umetokana na ushawishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo sanjari na wafanyabiashara hao, pia mameya wanane kutoka miji ya kisiwa cha Anjouan nchini humo wanatarajiwa kufanya ziara na kutembelea eneo la maonesho.

Wafanyabiashara hao wanawakilisha sekta zinazojishughulisha na biashara ya vifaa vya ujenzi, nguo, kampuni za maji, vinywaji, ufugaji, vyakula vya mifugo na bidhaa za kilimo hasa mazao ya mizizi.

Pia ilieleza kuwa wenyeji watapata fursa ya kujionea mbinu za uzalishaji na kuongeza thamani mazao ya vanila na langilangi kutoka kwa ushirika unaojishughulisha na uzalishaji wa mazao hayo ambayo ni muhimu kwa kampuni zinazotengeneza manukato.

SOMA: 2023: Idadi ya Watanzania yafika milioni 63.6

Alisema bidhaa za Tanzania zina soko kubwa Comoro na kuwa mahitaji makuu ni pamoja na zana za kilimo, mazao ya kilimo, nyama na wanyama hai na vyakula vya mifugo.

“Wafanyabiashara hao wameomba kupata fursa ya kufanya vikao na wafanyabiashara wa Tanzania katika maonesho hayo,” alisema Yakubu.

Habari Zifananazo

Back to top button