Wafanyabiashara 891 kurejeshwa sokoni Kariakoo
DAR ES SALAAM; MENEJIMENTI ya Shirika la Masoko ya Kariakoo, Dar es Salaam imetangaza orodha ya wafanyabiashara 891 wenye sifa na vigezo vya kurejeshwa sokoni Kariakoo baada ya ujenzi wa soko jipya na ukarabati wa soko kuu kukamilika.
Wafanyabiashara 164 katika orodha hiyo wamepangiwa kutumia eneo la soko kuu, 86 eneo la vigoli, 160 soko dogo la ndani, 146 soko dogo mzunguko, 123 soko la wazi na 212 eneo la shimoni.
Taarifa ya menejimenti hiyo kwa umma jana ilieleza kuwa wafanyabiashara wanaodaiwa na shirika ambao wapo kwenye orodha hiyo hawatarejeshwa sokoni hadi watakapolipa madeni ya kodi waliyolimbikiza kwa muda mrefu.
“Shirika linatoa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo tarehe 10 Julai 2024 hadi tarehe 09 Agosti 2024 kwa wadaiwa wote kukamilisha malipo ya madeni yao,” ilieleza taarifa hiyo.
Menejimenti imeeleza kuwa wafanyabiashara wenye hoja au maoni kuhusu majina yao kutoonekana kwenye orodha ya uhakiki wamepewa siku tatu kuanzia leo hadi Julai 13, mwaka huu kuwasilisha madai yao.
“Maafisa wa shirika watakuwepo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 9.00 alasiri kusikiliza na kutoa ufafanuzi kwa wafanyabiashara,” ilieleza taarifa.
Iliongeza: “Orodha hii pia imebandikwa kwenye mbao za matangazo zilizopo kwenye Soko la Machinga Complex na Soko la Kisutu”.
Soma pia:https://habarileo.co.tz/serikali-isiongeze-muda-ujenzi-soko-kariakoo/
Pia orodha ya wafanyabiashara hao ipo katika tovuti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na tovuti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo.
Akiwasilisha bungeni bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema wafanyabiashara zaidi ya 2,200 watapangwa katika jengo jipya la Soko la Kariakoo.
Mchengerwa alisema shirika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam walikuwa wanaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko jipya la Kariakoo lenye ghorofa sita za juu na ghorofa mbili za chini na ukarabati wa jengo kuu la soko la Kariakoo.
Alisema mradi ulianza kutekelezwa Januari, 2022 na mkandarasi Kampuni ya ESTIM Construction Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 28.03.
Mchengerwa alisema mtaalamu mshauri ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na alitaja maeneo yaliyoboreshwa ni kuwekwa kamera za kisasa za usalama, maeneo matatu ya benki na mashine nne za kutolea fedha na maduka ya kubadilisha fedha.
“Huduma hizi zitarahisisha shughuli za kifedha na hivyo kupelekea wafanyabiashara kutotembea na fedha umbali mrefu pamoja na maegesho ya magari 153,” alieleza Mchengerwa.