Wafanyabiashara waitwa maonesho Tunduma
SONGWE. Tunduma. MKUU wa Wilaya ya Momba, Kenani Kihongos amewakaribisha wawekezaji kutoka mikoa mbalimbali ndani ya nchi na wengine kutoka nchi jirani kutumia maonesho makubwa ya kibiashara ya siku tisa katika mji wa Tunduma wilayani Momba kutangaza biashara zao.
Amesema hayo wakati wa ufunguzi maonesho hayo makubwa ya kibiashara akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Songwe Dk Francis Michael na kueleza kuwa hiyo ni fursa kutangaza biashara zao.
” Sisi viongozi na wananchi wa Tunduma na Wilaya ya Momba tunawakaribisha wafanyabiashara na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu na nje ya nchi waje wafanye biashara, watoe elimu na kutangaza biashara zao na kufanya uwekezaji pia,” amesema.
Kuhusu ubora wa bidhaa Kihongos amewataka wafanya biashara kupeleka bidhaa zenye ubora ambazo zitaweza kushindana na bidhaa kutoka mataifa mengine jirani, ili kuongeza uchumi na Pato la Taifa.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ,Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA ), Charles Chenza, amesema maonesho hayo yatafungwa rasmi Oktoba 29 , 2023.