Wafugaji waonywa dhidi ya wakulima

RUVUMA: WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wafugaji kuishi kwa amani na kuheshimu sheria za nchi ikiwemo kuacha tabia ya kuingiza na kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

Waziri Ulega amesema hayo wakati wa kikao cha kusikiliza kero na changamoto za wafugaji wa Wilaya ya Namtumbo kilichofanyika jana.

Advertisement

“Wafugaji muishi na watu vizuri, acheni ubabe, fuateni sheria, msiingize mifugo katika mashamba ya watu kwa makusudi, ni jambo baya sana,, msipofuata sheria kila mtu mtamuona mbaya,” amesema.

SOMA: TALIRI yaja na ufumbuzi malisho kwa wafugaji

Waziri Ulega amewataka wafugaji hao kuunda mabaraza ya wazee ya wafugaji ili yasaidie kusuluhisha migogoro na kukemea wale wafugaji wachache wanaotaka kuharibu taswira ya ufugaji hapa nchini.

Katika hatua nyingine, Ulega amewaelekeza watalamu kutoka wizara yake kwenda kutoa elimu ya ufugaji bora na fursa zilizopo kwenye ufugaji kwa viongozi, wafugaji na makundi mengine katika wilaya hiyo ili wajue umuhimu wa uchumi jumuishi.