MAFUNDI wanaopata changamoto ya kuomba zabuni za ujenzi kwa kutumia mfumo wa kieletroniki wa manunuzi ya umma (NeST) wameagizwa kutoa taarifa kwa wataalam wa mfumo huo na waweze kuelekezwa jinsi ya kuutumia ili kuepuka miradi kukwama kwenye kata husika.
Aidha halmashauri ya Wilaya ya Arusha imetenga Sh milioni 45 kwa ajili ya ukarabati wa barabara mbalimbali zenye changamoto ili kuwezesha wananchi kuondokana na changamoto ya miundombinu kuharibika.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha DC, Seleman Msumi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichoshirikisha wataalam kutoka idara mbalimbali za halmashauri hiyo, madiwani pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa
Msumi amesema mfumo huo wa NeST ni mpya ambao unaelekeza zabuni mbalimbali kuombwa kupitia mfumo ingawa bado ni changamoto kwa mafundi wa kawaida kuutumia hali inayopelekea miradi mbalimbali kushindwa kuanza na na wakati mwingine fedha kurudi kutokana na mafundi hao kutojua kuutumia kuomba zabuni za ujenzi kwenye miradi mbalimbali inayotakiwa kujengwa kwenye kata.
“Tumebaini mfumo huu bado ni changamoto kwa mafundi wetu hawa wadogo hivyo tunaomba ushirikiano pale wanapokwama kuomba zabuni wataalam wapo watawasaidia ili kupeuka miradi kukwama ilhali sifa wanazo lakini hawajui jinsi ya kutumia mfumo manunuzi”.