Wagombea CCM waahidi kliniki za kibingwa

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Geita mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhandisi Chacha Wambura amesema akichaguliwa anatamani kuona kliniki za madaktari bingwa zinafika vituo vya afya.
Mhandisi Chacha amesema hayo wakati akinadi sera na kuomba kura za chama hicho katika kata ya Nyanguku iliyopo Manispaa ya Geita kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025. Amesema iwapo atapewa rdihaa ya kuwa mbunge wa jimbo la Geita mjini atashawishi uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kupanga utaratibu wa madaktari bingwa kufanya kliniki kwenye vituo vya afya.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza adha ya wananchi kutumia gharama kubwa kufuata vipimo na matibabu ingali tayari serikali inatumia gharama kubwa kujenga miundombinu ya vituo vya afya. Amesema ilani ya CCM 2025-2030 inaonyesha tayari serikali imeshatenga kiasi cha sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Nyankungu ili kusogeza huduma bora za afya.
Aidha Mhandisi Wambura amesema bado pia kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha Manispaa ya Geita inakuwa kinara kwenye sekta ya elimu kwa kuhakikisha ubora wa elimu unaendana na majengo yaliyopo. “Tuna mpango wa kuhakikisha Geita (Manispaa) inaongoza kwa suala la elimu, tunataka tuongoze hapa Geita (mkoa) harafu wengine wafuate”, amesema Mhandisi Wambura.
Mgombea Udiwani wa CCM kata ya Nyanguku, Elias Ngole amekiri kuwa kwa sasa kazi kubwa imefanyika kujenga majengo ya kisasa kwenye zahanati na vituo vya afya lakini kuna uhitaji mkubwa wa matabibu. “Sipendi tujenge kituo cha afya kwa maana ya majengo, naomba tukajenge kituo cha afya kwa maana ya huduma, tukalete madaktari bingwa”, amesema Ngole. SOMA: Mwinyi: Hakuna atakayebaguliwa, wote ni wazanzibari



