Wagombea urais, ubunge wabanwa fedha za uchaguzi

DODOMA : WAGOMBEA urais, ubunge na udiwani wanatakiwa kutangaza fedha walizonazo kwa ajili kwa kugharamia uchaguzi. Sheria ya Gharama za Uchaguzi inawataka wafanye hivyo ndani ya siku saba tangu wateuliwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Aidha, sheria inavitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kumjulisha Msajili wa Vyama vya Siasa fedha walizopanga kutumia kugharimia uchaguzi zikiwemo fedha zitakazotumiwa na wagombea wao kugharimia uchaguzi.
Sheria inavitaka vyama vifanye hivyo ndani ya siku 30 tangu siku ya uteuzi. Agosti 27, mwaka huu, INEC iliteua wagombea 17 wa urais, ubunge katika majimbo 272 na wa udiwani hivyo siku hizo za kisheria zinatimia keshokutwa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi sura namba 278 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015, wagombea urais wanapaswa kutoa taarifa hizo kwa makatibu wakuu wa vyama vilivyowapitisha wagombee nafasi hiyo. SOMA: Mgombea urais ukomo gharama bil 9/-
Sheria inataka wagombea wa ubunge na udiwani wawasilishe taarifa hizo kwa makatibu wa vyama vyao wa wilaya pia wakieleza fedha wanazotarajia kuzipata na kuzitumia kugharimia uchaguzi. Kwa mujibu wa sheria hiyo, kitendo cha wagombea kutangaza fedha zao za kugharamia uchaguzi utakuwa ni uthibitisho kuwa wamekubali sharti hilo.
Sheria inaeleza kwamba makatibu wakuu wa vyama na makatibu wa vyama wa wilaya watatoa vyeti kuonesha wagombea wametekeleza sharti la kutangaza fedha zao za kugharimia uchaguzi. Inaeleza kuwa viwango vitakavyotangazwa vitakuwa siri isipokuwa kama vitahusishwa na malalamiko ya Msajili wa Vyama vya Siasa, uchunguzi ulioanzishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa au mwenendo wa kesi mahakamani.
Sheria inaeleza, kama mgombea au chama cha siasa kitatumia zaidi ya kiwango walichoeleza watapaswa kuandika ripoti kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakieleza sababu za kutumia fedha zaidi ya walizoeleza.



