Wagonjwa kuelekea Muhimbili wapungua Moro

MOROGORO: IDADI  ya rufaa ya wagonjwa kutoka Hospitali ya Rufaa Morogoro kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepungua.

Hatua hiyo imetokana na uwekezaji mkubwa na uboreshaji miundombinu ya kutolea huduma za afya na magonjwa ya dharura uliofanywa na serikali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Kabla ya kufanyika mambo hayo,hospitali hiyo ilikuwa inapeleka wagonjwa Muhimbili na kanda kati ya 70 hadi 80 lakini kwa sasa idadi hiyo imepungua na kufikia wagonjwa wasiozidi 30 hadi 40 kwa mwezi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo, Dk Daniel Nkungu amesema hayo alipotoa taarifa baada ya ukarabati wa miundombinu ya jengo la kliniki maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali uliofanywa kwa msaada wa fedha kiasicha sh milioni 18 zilizotolewa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ( WCF).

Dk Nkungu amesemahospitali ya rufaa hiyo kwa sasa inatoa za huduma ya magonjwa mbalimbali kupitia vipimo vya kisasa kikiwemo cha CT Scan, Digital X-Ray, Mtambo wa kufua hewa tiba ya oksjeni, kifaa cha kuchunguza sikio, koo, pua, mashine kumi za kuchuja damu (Dialysis) na uboreshaji wa huduma za daraja la kwanza.

“Miaka ya nyuma huduma hizi hazikuwemo na hivyo kama hospitali tulilazimika kuwapa rufaa wagonjwa wetu ya kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali nyingine za rufaa za kanda” amesema Dk Nkungu.

“ Lakini kwa sasa wagonjwa tunaopokea kutoka kwenye hopsitali za wilaya ni zaidi ya 2,000 kwa mwezi na rufaa tunazotoa kwa mwezi hazizidi 40 mwa mwezi hapa mtaona namna hospitali yetu ilivyoboreshwa,” amesema Dk Nkungu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk John Mduma amesema ukarati huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kipaumbele cha kuboresha sekta ya afya nchini.

“Tumeona tufanye hivi kwa sababu hospitali ni moja ya taasisi ambazo tunashirikiana nazo kwa karibu katika majukumu yetu ya kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata ajali ama ugonjwa wakiwa mahala pa kazi,” amesema.

“Hospitali ni moja ya sekta ambazo tunazitumia katika kujua ukubwa wa ugonjwa ama madhara aliyoyapata mfanyakazi akiwa mahala pa kazi kabla ya kumlipa fidia,” amesema Dk Mduma.

Dk Mduma amesema  mfuko huo unapotekeleza sera yake iliyopitishwa na Serikali ya kurudisha sehemu ya fedha ya michango yake kwa umma na hospitali hiyo ni moja ya eneo lililoangaliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button