Wahitimu JKT wapewa kipaumbele ajira

KAMATI maalum inayozishirikisha sekta mbalimbali za uzalishaji imeundwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa wahitimu wanaomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanapata ajira.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa ameweka wazi hilo leo bungeni, wakati akijibu maswali ya nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Malinyi, Antipas Mgunguzi, aliyetaka kujua hatua iliyofikiwa na serikali katika kutekeleza agizo la mwaka 2013 la kutoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu wa JKT.

Aidha Mbunge huyo alitaka kujua sababu za kutoajiri wahitimu kwa kutoa kipaumbele kwa wahitimu wa awali kabla ya wapya ili kutowavunja moyo.

Hata hivyo, Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa kamati iliyoundwa kwa kushirikisha wizara za uzalishaji ni kuhakikisha ahadi ya jumla ya ajira milioni nane zilizoelezwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inatekelezeka.

Katika majibu yake kwa swali la msingi, Bashungwa amekiri kuwa mnamo mwaka 2013, Serikali ilitoa maelekezo kwa wizara zote za Serikali pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana waliohitimu mafunzo ya  JKT na limekuwa likitekelezwa tangu lilopotolewa.

Hata hivyo Waziri amesisitiza kuwa lengo la mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwapatia vijana wa Tanzania elimu ya uzalendo, ujasiriamali na kujifunza stadi za kazi ili waweze kujiajiri mara wamalizapo mafunzo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button