WANANCHI wa Kijiji cha Kimange wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wameiomba serikali kuwapatia dawa ili waweze kuwadhibiti wadudu aina ya viwavijeshi vamizi ambao wamevamia mashamba yao hususani zao la mahindi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimange, Said Bakari wakati walipotembelewa na watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania ( TARI), Kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa mkoani Morogoro kujionea hali halisi ya tatizo hilo.
Bakari amesema wadudu hao wa viwavijeshi vamizi ambao katika kijiji hicho wanawaita sondo wamekuwa wakiwasumbua hivyo kwa wenye uwezo wamekuwa wakinunua dawa na kupuliza ila wasiokuwa nao wamewaacha waendelee kushambulia.
“Mwaka jana imesababisha njaa mpaka sasa hivi watu wana njaa kwa sababu ya huyu mdudu Sondo alishambulia sana. Kwa sasa kuna mashamba yameathiriwa sasa yule mwenye uwezo kidogo ndio anawadhibiti, wale ambao uwezo wao mdogo ndio tunatoka patupu,” amesema.
Amesema endapo pembejeo zingekuwa karibu ingekuwa rahisi mkulima anapoona dalili za wadudu hao anadhibiti mapema.
Naye Mkulima Juma Ngowe amesema kila siku anapokagua shamba anakuta wadudu hao ambao wanasababisha uharibifu mkubwa.
Kwa upande wake Mratibu wa Utafiti, Kilimo na Ubunifu kutoka TARI Ilonga, Meshack Makenge amesema wamefika katika kijiji hicho kuangalia ukubwa wa tatizo waweze kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na viwavijeshi vamizi hao, kwa kuwa ili kumdhibiti elimu ya kumtambua inahitajika.
” Inatakiwa elimu kuelimisha wananchi namna ya kupambana naye hususani kiasi cha kupiga dawa, kiasi cha maji na muda wa kupiga dawa. Hicho kitu ni muhimu sana,” amesema na kuongeza kuwa pia wanatoa elimu ya kumtambua huyo mdudu.
Amesema zikitumika dawa sahihi na viwango sahihi vya kuchanganya maji na muda wa kuipiga inakuwa rahisi kumdhibiti.
Amesema kanuni bora zikifuatwa mkulima anapata mazao mengi katika shamba la hekta moja, kwani atapanda mimea 4,444, gunzi la mahindi linakuwa na mistari 14 na punje zake 52, matokeo yake mkulima atapata za kutosha.
Naye Mratibu za Zao la Mahindi Kitaifa kutoka TARI Ilonga, Dk Arnod Mushongi ambaye naye alifika katika kijiji hicho kuangalia hali halisi ya ukubwa wa tatizo, amesema kikubwa kinachotakiwa ni maofisa ugani kushirikiana na wakulima ili kubaini tatizo mapema.
Amesema alichokiona ni kwamba tatizo linakuwa kubwa kutokana na wakulima kukosa elimu ya kufuata kanuni za kilimo bora na elimu ya kumtambua na kumdhibiti mapema mdudu huyo hatari kwa mazao.
” Mdudu huyu ana uwezo mkubwa sana. Ana uwezo wa kwenda kilomita 2000, anaweza kutaga mayai zaidi ya 1000, anaweza kujibadili na kujificha usimuone, pia ana mbinu nyingi za kumfanya aweze kuishi.
” Mdudu huyu anaweza kusababisha mkulima asipate mavuno kabisa au akasababisha mahindi yakaoza na kutengeneza sumu,” amesema.
Amesema inapaswa kuangalia njia mbalimbali za kumdhibiti kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, kupanda kwa nafasi, kutumia mbegu bora pamoja na kuandaa shamba mapema.
Amesema kiwavijeshi vamizi amekuwa akisababisha madhara kwa sababu ni mdudu mpya ameingia nchini 2017 akitokea Amerika ya Kusini na Kati.