Wakimbia makazi baada ya ‘kumuua’ mkulima

WANANCHI wa Kitongoji cha Katani, Kijiji cha Nguru wilayani Igunga, Tabora wameyakimbia makazi yao kwa kuhofia kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mkulima Kushoka Maganga (40) kwa kumshambulia kwa fimbo, mawe na marungu.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nguru, Igunda Kuhenga alisema tukio la kuuawa mkulima huyo ni la Septemba 11, mwaka huu baada ya kundi la wananchi zaidi ya 300 wa kitongoji hicho waliotambulika kwa jina la Jeshi la Jadi Sungusungu kudaiwa kumshambulia.

Alieleza watu hao walijikusanya na kumshambulia mkulima huyo kwa marungu, fimbo na mawe wakimtuhumu kuiba ng’ombe mmoja kwa mfugaji ambaye hawakumtaja jina ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Bulumbela, Kata ya Ziba.

Advertisement

Kuhenga alisema pamoja na mkulima huyo kujitetea kutokuhusika na wizi wa ng’ombe huyo lakini wananchi hao waliendelea kumshambulia hadi kufariki na baada ya hapo walikimbia kusikojulikana.
“Kwa kweli huyo mkulima wamemuonea kwani mimi namfahamu vizuri, hana tabia hiyo ya wizi ila kwa kuwa alitajwa na mtu, hicho ndicho kimesababisha auawe. Hata hivyo wananchi walipaswa wafanye uchunguzi kwanza,” alisema Kuhenga.

Alieleza mwananchi huyo amezikwa Septemba 12, mwaka huu mchana na wananchi wa Kitongoji cha Katani walioshiriki mauaji hawakuhudhuria kwani walikimbia, nyumba zao zimebakiwa na wanawake na watoto tu.

Nao baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo huku wakigoma kutaja majina yao, walisema walishuhudia mwananchi huyo akishambuliwa huku akiomba msaada huku akijitetea kuwa si mwizi na mwisho alisema, “Mmeamua kuniua bila kosa.”

Soma pia: Mauaji Njombe yaacha maswali, Polisi wajitosa

Mwananchi huyo alisema, “Sisi tulishuhudia kwa macho wakati akikata roho na ndiyo maana hatujakimbia na tumeshiriki mazishi hivyo tunaomba wote walioshiriki mauaji na kukimbia watafutwe na wafikishwe mahakamani,” alisema mmoja wao.

Diwani wa Nguru, Yasinta Ngassa (CCM) alikiri kuuawa kwa mwananchi huyo na kuongeza kuwa mpigakura wake wamemuonea kwani hana tabia ya wizi.

Alisema Jeshi la Polisi Igunga limekuwa likitoa elimu mara kwa mara kwa wananchi kutojichukulia sheria mikononi lakini wamekuwa wagumu kuelewa hivyo wanapaswa kukamatwa wote waliohusika na kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Constantine Mbogambi alithibitisha kuuawa kwa mkulima huyo na kueleza wananchi hao walichukua uamuzi huo baada ya kumtuhumu kwa wizi.

Alisema Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika wote wa mauaji hayo.