DODOMA: MBUNGE wa Hai, Saashisha Mafuwe, ameiomba Serikali iruhusu wanaume kunufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kama ilivyo kwa wanawake na vijana, akisema kumekuwepo na malalamiko makubwa kutoka kwa wanaume kwa kutokupata fursa hiyo.
Mafuwe ameeleza kuwa anaiunga mkono Serikali kwa juhudi zake za kuratibu utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, ambapo asilimia 4 inatolewa kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana, na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.
Alisema hivi karibuni kumefanyika maboresho ya kanuni, yakiwemo kuongeza umri wa vijana kutoka miaka 35 hadi 45, jambo ambalo alikili ni muhimu.
“Kundi la wanaume limeachwa nyuma. Hivyo, je, Serikali haioni kuwa ni wakati sahihi sasa kuruhusu wanaume nao wanufaike na mikopo hii?,” aliuliza Mafuwe.
Mafuwe aliongeza kuwa, “Serikali haioni umuhimu wa kufanya marekebisho ya kikanuni ili wanaume nao wanufaike, bila kigezo cha umri?”. SOMA: Mvomero wafanya kweli mikopo asilimia 10
Akijibu swali hilo,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema upatikanaji wa mikopo katika maeneo mbalimbali ulifanyiwa tathmini, ambapo iligundulika kwamba baadhi ya makundi hayakuwa na fursa nzuri.
Hali hiyo ilichangia kuanzishwa kwa mikopo maalumu kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu.
“Tuliona kwamba baadhi ya makundi, ikiwemo wanawake na walemavu, hawakuwa na fursa nzuri ya kupata mikopo, ndiyo maana tulianzisha mikopo maalumu kupitia halmashauri zetu” alisema Waziri Mkuu .
Aliongeza, “Vijana walipokuwa na umri wa miaka 35, wanaume waliokuwa vijana walikuwa na fursa ya kukopa, lakini baada ya miaka 35 walikuwa na nafasi ya kwenda kwenye taasisi za kifedha. Tathmini yetu inaonyesha kuwa wanaume wengi wanapata mikopo kupitia taasisi za kifedha kuliko wanawake,” Alimalizia.