MOROGORO: WALIMU zaidi ya 200 kutoka shule za msingi katika wilaya tatu za mikoa ya Pwani, Njombe na Morogoro wamejengewa uwezo wa kutumia mbinu rafiki za ufundishaji wa stadi za kusoma , kuandika na kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi kupitia Mradi wa ‘Kijiji Changu’ uliotekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali Uwezo Tanzania.
Meneja wa Mawasiliano wa Shirika hilo , Greyson Mgoi amesema hayo mjini Morogoro kwenye mkutano wa kutathimini utekelezaji wa mradi na kushirikisha baadhi ya walimu , Maofisa Elimu ya Awali na Msingi wa Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, Kisarawe mkoani Pwani na Ludewa katika Mkoa wa Njombe.
Mgoi amesema mradi huo licha ya kuwajengea uwezo walimu pia umewafikia wanafunzi zaidi ya 7,000 katika shule zilizopo kwenye vijiji 100 vilivyopo katika wilaya hizo.
Amesema Shirika hilo linatekeleza jitihada mbalimbali zinazolenga kusaidia watoto kupata kujifunza, kuchangia katika ubora wa elimu kwa kushirikiana na wadau kuboresha elimu na sera.
Mgoi amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka 2022 na umefikia tamati Desemba mwaka jana (2023),na ulilenga kupunguza changamoto za wanafunzi wanaoshindwa kumudu vyema stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa baadhi ya wanafunzi wa wilaya hizo.
Amesema kabla ya kuanza mradi maeneo hayo wanafunzi walipimwa walionekana kushindwa kumudu vyema stadi hizo , lakini kwa sasa wameongeza uwezo wa ufauli wa kusoma , kuandika na kuhesabu.