Walipa kodi 4,696,999 wamesajiliwa na TRA

DODOMA; SERIKALI imesema hadi kufikia Juni 30, 2023 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilikuwa imesajili jumla ya walipa kodi 4,696,999, sawa na asilimia 16 ya idadi ya nguvu kazi iliyopo nchini ambayo ni takribani watu milioni 33.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi(BLW), Ameir Abdallah Ameir, aliyetaka kujua ni asilimia ngapi ya wafanyabiashara hawajaingizwa katika mfumo rasmi wa kodi na Serikali inachukua hatua gani kuwafikia.

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Naibu Waziri Kigahe amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupanua wigo wa kodi.

“Hadi Juni 30, 2023 Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikuwa imesajili jumla ya walipa kodi 4,696,999, sawa na asilimia 16 ya idadi ya nguvu kazi iliyopo nchini ambayo ni takribani watu milioni 33.

“Idadi ndogo ya usajili wa walipakodi, ikilinganishwa na fursa ya nguvu kazi iliyopo inatokana na sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi hapa nchini kuendeshwa na sekta isiyo rasmi inayokadiriwa kuajiri takribrani watu milioni 27.7.

“Mheshimiwa Spika, hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kurasimisha sekta isiyo rasmi ni pamoja na kampeni ya mlango kwa mlango inayolenga kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara wasiotambulika, kutenga na kujenga maeneo maalumu ya masoko kwa wafanyabiashara wadogo na kuendelea kutoa elimu na ufafanuzi wa kina kwa wananchi kuhusu masuala ya kodi, ili kuhamasisha wananchi kurasimisha biashara na shughuli za kiuchumi kwa hiari,” amesema Naibu Waziri Kigahe.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button