Wamiliki wa migodi Mirerani wafundwa
MWENYEKITI wa Kamati ya Usuluhishi na Usalama katika Migodi ya Tanzanite iliyopo katika Mji wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Charles Chilala amewataka wamiliki wa migodi hiyo kuheshimu maamuzi ya kamati wanapoamua migogoro wa kuingiliana ndani ya migodi (Mitobozano) ili kulinda amani na usalama migodini.
Hatua hiyo imefuatiwa malalamiko kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Njake Enterprises and Oil Transport inayechimba Madini ya Tanzanite katika kitalu B Mirerani, Japhet Lema kwa kuilalamikia Kampuni ya Gem & Rock Venture ambapo Septemba 2 wafanyakazi wa kampuni hiyo walilipua baruti na uchorongaji eneo lililositishwa na kamati na kuhatarisha amani kwa wafanyakazi wake na kuiomba kamati kuchukua hatua dhidi ya kampuni hiyo.
SOMA: ‘Kagueni migodi kwa faida, usalama zaidi’ – …
Mwenyekiti wa Kamati amesema kamati iko kisheria na inatambulika na Wizara ya Madini hivyo aliwaomba wamiliki wa migodi kuheshimu maamuzi ya kamati vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria pindi wanapozarau maamuzi ya kamati.
Chilala alisema Meneja wa Gem & Rock Venture aliitwa katika ofisi ya Wizara ya Madini Mirerani na kuonywa kuheshimu maamuzi ya kamati kwa kuwa kamati hiyo iko kisheria na wakiendelea kukaidi wanaweza kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa mgodi.
Alisema kamati iligundua vitu vingi katika Mgogoro wa Njake na Gem & Rock na kamati ilimwagiza meneja wa kampuni ya Gem & Rock watafute sehemu nyingine ya kufanyia kazi ambayo ni salama na pia kamati iliiamuru kampuni hiyo kuacha kufanya kazi katika eneo hilo hatua ambayo iliamuliwa na wajumbe nane kati ya tisa wa kamati hiyo.
SOMA: Waitahadharisha serikali harufu ya upigaji migodini
‘’Tunataka amani na usalama katika migodi ya Tanzanite Mirerani hivyo kila mmiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite anapaswa kutii maagizo ya kamati ikiwa ni pamoja na kuwaagiza mameneja wao kufuata sheria na kanuni na sio vinginevyo,” alisema Chilala
Naye Ofisa Madini Mfawidhi wa Wizara ya Madini Mirerani, Nchangwa Chacha alipoulizwa juu ya ukaidi uliofanywa na kampuni ya Gem & Rock Venture wa kudharau maamuzi ya kamati alisema kuwa suala hilo limemalizwa na maelekezo yameshatolewa kwa wahusika mengine yamebaki kwa taratibu za kiofisi.
Chacha aliwahimiza wamiliki wa migodi kuitambua na kuiheshimu kamati kwani imechaguliwa kisheria na iko kisheria hivyo wote wanapaswa kutii maamuzi yake ili uchimbaji wa madini ya Tanzanite ufanywe kwa kuzingatia sheria na kanuni kuepuka maafa yasiyokuwa ya lazima.
Japhet Lema Mkurugenzi wa Kampuni ya Njake amesema kuwa wafanyakazi wa kampuni ya Gem & Rock wamekuwa na tabia ya kukaidi maagizo ya kamati na kurudiarudia makosa yale yale hivyo aliomba kamati na ofisi ya Wizara ya Madini Mirerani kutoa makucha na kutoa adhabu stahiki ili tabia hiyo isiweze kujirudia tena.
Apoulizwa Mkurugenzi wa Gem & Rock Venture,Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti juu ya kukaidi maamuzi ya kamati alisema sio kweli ila wafanyakazi wa Njake ndio waliovamia mgodi wake na kupora madini na kujeruhi baadhi ya wafanyakazi na kusema kuwa taarifa zote anazo Chacha Ofisa Mfawidhi Wizara ya Madini Mirerani lakini Chacha alipoulizwa alisema hakukuwa na kitu kama hicho katika uchunguzi wao wa awali na kusema kuwa ulikuwa uzushi tu.