Wanachuo 17 mbaroni kumng’oa meno mlinzi

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amethibitisha kukamatwa kwa wanachuo 17 wa Chuo cha Ardhi tawi la Tabora kwa tuhuma za kumpiga mlinzi wa chuo hicho na kumng’oa meno manne.
Kwa mujibu wa Chacha, wanachuo hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Tabora kufuatia tukio hilo, huku wengine wawili wakikutwa na silaha aina ya kisu katika eneo la bweni lao, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za chuo.
Amesema jina la mlinzi aliyejeruhiwa limehifadhiwa kwa sasa wakati uchunguzi ukiendelea. Chacha ameuagiza uongozi wa chuo hicho kuwasimamisha masomo wanachuo hao pamoja na kuhakikisha wanachukuliwa hatua za kisheria kwa kufunguliwa mashitaka. SOMA: Mbunge Salim Hasham awapa neno wanafunzi wa vyuo Morogoro
Aidha, amewataka wanafunzi wengine wa vyuo kuepuka kuiga vitendo vya uhalifu na badala yake kujikita katika masomo yao yaliyowapeleka chuoni. “Vyuo ni maeneo ya kujifunza na kujenga mustakabali wa maisha, siyo kufanya vitendo vya uhalifu,” alisisitiza.



