Wanafunzi DIT kupata fursa
DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC), imetoa mafunzo kwa vitendo ya masuala ya ujenzi kwa wahitimu watarajiwa katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ( DIT), ili kuwaongezea ujuzi.
Naibu Meneja wa Kampuni ya CCCC, Liyuliang Lee amesema hayo walipowatembelea wanafunzi wa DIT mkoani Dar es Salaam.
Amesema kampuni hiyo imekuwa ikiwachukua vijana wanaotarajiwa kuhitimu ili kuwaimarisha kivitendo, imani yao baada ya miaka mitano mpaka 10, wanafunzi hao wayakuwa na ujuzi wa hali ya juu kwa taifa la Tanzania na nchi nyingine.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Viwandani kutoka DIT, Dk Sosthenes Karugaba amesema taasisi hiyo ya kichina imekutana na wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu ili wawaeleze kuhusu shughuli wazifanyazo pamoja na walizonazo kwenye miradi yao mbalimbali.
SOMA: DIT kutengeneza vipuri vya vyombo moto, mitambo
“Wamekutana na wanafunzi wa Uhandisi, Sayansi na Teknolojia ili kuwaeleza wanatarajiwa kuwaje, wakiingia katika ulimwengu wa kujiajiri au kuajiriwa,” amesema.
Amesema mafunzo hayo ya vitendo yanasaidia wanafunzi kuwajengea uthubutu pindi wanapohitimu, wanakuwa na sifa zote za kufanya kazi kivitendo zaidi.
Naye Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye ni Meneja Msaidizi Kitengo cha Mashine na Malighafi katika kampuni hiyo ya CCCC, Edson Edward amesema kampuni hiyo inawatafuta wanafunzi bora na wale wanaojituma ili kuwaandaa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya vitendo, tofauti na nadharia.