Wanafunzi sekondari Kiluvya wafikiwa msaada wa kisheria

DAR ES SALAAM: TIMU ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafikia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiluvya wilayani Ubungo Dar es Salaam na kuwaelimisha masuala mbalimbali ikiwemo jinsi ya kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza leo Juni 18,2025 shuleni hapo, mwanasheria katika timu hiyo, Nipael Ezekiel aliwaambia wanafunzi hao kuwa wanapaswa kutoa taarifa iwapo watafanyiwa vitendo vya ukatili katika jamii.
“Msinyamaze,mnapofanyiwa vitendo vya ukatili ambavyo nimevitaja (kupigwa, kuchomwa, kubakwa, kulawitiwa, kufungiwa ndani na vitendo kama hivyo aua nyumbani ,mtaani au shuleni toeni taarifa polisi,kwenye ofisi ya serikali ya mtaa au kwa jirani ambaye anaweza kulifikisha kwenye mamlaka husika,”amesema Nipael.
Kampeni hiyo imezinduliwa juzi mkoani humo ikiwa ni mkoa wa mwisho kati ya mikoa 31 nchini iliyofikiwa na huduma hiyo ambayo imetajwa kuwa mkombozi kwa wananchi kwakuwa inatoa bure elimu na msaada wa kisheria.
Hata hivyo mwito umetolewa kwa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa katika kata zote 10 za wilaya hiyo. Leo ni zamu ya Kata ya Kibamba na Goba.