WANAFUNZI 600 kutoka vyuo mbalimbali vya Mkoa wa Dar es Salaam, wamejitokeza leo katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kuchangia damu, huku chupa 400 zikitarajiwa kukusanywa katika uchangiaji huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa MOI, Dk Respisius Boniface alisema mahitaji ya damu ni chupa 25 hadi 30 kwa siku na kwa wiki ni chupa 150.
“Niwashuku wanafunzi wa vyuo na wadau mbalimbali hususani Azim Dewji kwa kuchangia gharama zinazotumika leo, damu ni kujitolea sio kidonge kinunuliwe haipatikani, hivyo ni jambo la msingi sana,” amesema.
Amesema katika taasisi hiyo wanafanya upasuaji mkubwa kwa wagonjwa mbalimbali, kama vile mifupa, ubongo ajali za magari, pikipiki pamoja na matibabu mengi, hivyo lazima mgonjwa apate damu.
Amefafanua kuwa kwa siku wanapokea majeruhi 10 hadi 15 wa ajali za barabarani na kati yao asilimia 70 ni majeruhi wa ajali za bodaboda.
“Damu tunapata kwa asilimia 87 kwa sasa hapo katikati hali ilikuwa ngumu na sasa mwamko umerudi, hivyo hawa wanaokoa Watanzania wenzetu na Watanzania wawe na moyo huu wa kujitoa,”ameeleza Dk Boniface.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MOI, Patrick Mvungi, amesema licha ya wanafunzi hao kuchangia damu pia wanapewa elimu ya umuhimu wa bima ya afya kwa wote.
“Na pia vijana hawa wamepata elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya na watakuwa mabalozi wazuri katika jamii,” amesema.
Naye Kaimu Mkuu kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Neema Mwangomo amesema
Muhimbili wanatumia chupa 150 lakini wanapata chupa 50 hadi 60.
Amesema wanaohitaji damu ni wagonjwa wa saratani, watoto wenye saratani, wajawazito, wagonjwa wa upasuaji na wengine.