Wananchi Bukoba wahimizwa kutunza barabara

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava amewataka wakazi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wanaotumia barabara ya mtaa wa Kashabo kuitunza na kuhifadhi vizuri kwa faida endelevu ya watumiaji.

Kiongozi huyo ametoa wito huo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi kwenye mradi huo unaounganisha Hamugembe, Bakoba na Rwamishenye yenye urefu wa kilomita 0.7 iliyofikia asilimia 98 na kuonesha kuridhika na utekelezaji wa mradi huo.

Advertisement

SOMA: Mwenge wa Uhuru kukagua miradi ya Sh bilioni 1 Ukerewe

“Mwenge wa Uhuru umeridhika na utaweka jiwe la msingi, barabara hii iendelee kutunzwa na kuhifadhiwa vizuri ili itumike kwa usafiri na usafirishaji kwa muda mrefu kwa wananchi wa Manispaa ya Bukoba lakini pia viwango ambavyo vinatarajiwa,” amesema Mnzava.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Bukoba, Andondile Mwakitalu amesema kuwa mradi huo umegharimu Sh milioni 437 na baada ya kukamilika utawanufaisha wananchi wa kata ya Hamugembe na maeneo jirani kwa kupunguza adha ya usafiri na usafirishaji.

SOMA: Mwenge wa Uhuru wakagua miradi ya Sh Bil 5 Iramba

“Baada ya kukamilika tunatarajia mradi huu uwe na faida kwa wananchi wa Bukoba kwa ujumla kwa usafiri na usafirishaji lakini pia kupunguza adha ya tope na vumbi kwa wananchi wanaoishi karibu na barabara hii,” amesema Mwakitalu.

Baadhi ya wananchi na viongozi wa maeneo hayo akiwemo, Frolian Rutta amesema kabla ya kutengenezwa barabara hiyo hapakuwa na mkondo maalum wa kusafirisha maji hali iliyosababisha nyumba zao kujaa maji yaliyokuwa yakisafiri kutoka milimani.

“Wananchi wa Maeneo haya tulikuwa tunapata shida sana maji yalikuwa yanaingia mpaka majumbani lakini pia hapakuwepo na mikondo au mitaro maalum ya kusafirisha maji kwakweli lilikuwa ni tatizo kubwa,” amesema Rutta.

Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Steven Byabato amesema kuwa kata ya Hamugembe imenufaika kwa barabara hiyo kutoka kiwango cha changalawe Hadi kiwango cha lami kwani maeneo hayo yalikuwa na changamoto ya kupitika hasa nyakati za msimu wa mvua.

“Maeneo haya yamekuwa na changamoto sana hasa wakati wa mvua mashimo yanakuwa mengi lakini kwa sasa karibia asilimia 70 barabara za hii kata zimekiwa kwenye kiwango cha lami,” amesema Byabato.

Mradi huo wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 0.7 utekelezaji wake ulianza Oktoba 13, 2023 na unatarajia kukamilika Oktoba 15, 2024 kwa gharama za Sh milioni 437.