Wananchi Pagwi waiomba Serikali kukamilisha zahanati

TANGA: WANANCHI wa Kijiji cha Pagwi, wilayani Kilindi, mkoani Tanga, wameiomba Serikali kusaidia kukamilisha ujenzi wa zahanati yao ulioanza mwaka 2018 kwa nguvu zao wenyewe, wakieleza kuwa ukosefu wa huduma za afya karibu umekuwa changamoto kubwa, hususan kwa wanawake wajawazito.
Wananchi hao walisema hulazimika kutembea takribani kilomita nne kufuata huduma za afya katika vijiji jirani, huku hali ya barabara ikiongeza ugumu wa kuwafikisha wagonjwa hospitalini kwa wakati.

Walisema changamoto hiyo imekuwa na madhara kwa wajawazito, ambapo ndani ya mwaka huu wanawake watatu wamejifungua njiani wakati wakielekea kutafuta huduma za afya.
Akijibu kero hiyo, Mtendaji wa Kata ya Pagwi, Mustapha Msingwa, alisema Halmashauri tayari imetenga Sh milioni 20 kwa ajili ya kusaidia kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilindi, Saleh Mhando, alisema kiasi kingine cha shilingi milioni 30 kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.

Katika kuunga mkono juhudi za wananchi, Mhando ametoa shilingi laki tano pamoja na mifuko 50 ya saruji, ambayo itatumika katika hatua ya upigaji lipu ya jengo hilo.
Wananchi hao sasa wanasubiri kukamilishwa kwa fedha zilizotengwa na Halmashauri ili ujenzi wa zahanati hiyo uweze kukamilika na kuwawezesha kupata huduma za afya karibu na makazi yao.



