WANANCHI mkoani Morogoro wameonesha kitendo cha uzalendo kwa kuchangia kiasi sha Sh milioni 280.9 kati ya Sh bilioni 12 .1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ,Fatma Mwassa alisema hayo katika hotuba yake ya mapokezi na makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa , Halima Dendego katika sherehe iliyofanyika jana ( Mei 6, 2023), kata ya Chita , Halmashauri ya Mlimba Wilaya ya Kilombero.
Mwassa alisema Mwenge wa Uhuru utapitia jumla ya miradi 68 yenye thamani ya Sh bilioni 12,1 kwa ajili ya ufunguzi, uzinduzi, uwekaji mawe ya msingi na kukagua , hivyo miradi 24 itawekewa jiwe la msingi, mitano itafunguliwa, 19 itazinduliwa na miradi 20 itakaguliwa.
Mkuu wa mkoa alisema kati ya fedha hizo , wananchi wamechangia kiasi cha sh milioni 280.9, halmashauri Sh bilioni 2.014 ,serikali kuu Sh bilioni 7.8 na wahisani na Asasi mbalimbali Sh bilioni 2.031.
Mwassa aliwapongeza wananchi wa mkoa huo kwa kuonesha moyo wao wa uzalenzo kuchangia fedha na nguvu kazi kwenye miradi ya maendeleo na ikia ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea maendeleo yao .
Mkuu wa mkoa alitaja ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 ni : “ Kuhifadhi Mazingira na kutunza vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa” .
Ujumbe huo unaambatana na kaulimbiu ya : “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa”.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilainza jana katika halnmashauri ya Mlimba iliyopo wilaya ya Kilombero , na baadhi ya miradi iliyopitiawa ni ujenzi wa wodi ya Mama na Mtoto na Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya Chita kilichopo kata ya Chita.
Katika taaifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo , Mhandisi Stephano Kaliwa iliyosomwa mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Kitaifa, Abdallah Shaib Kaim , kuwa jengo la Mama na Mtoto ambalo bado ujenzi unaendelea hadi sasa zimetumika Sh milioni 150.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kuwa mradi huo ulianza kujengwa mwishoni mwa mwezi julai, 2022 na umelenga kurahisisha na kusaidia huduma za Mama Wajawazito na kuondoa vifo vya Mama na Mtoto kwa wananchi wa kata ya Chita na maeneo ya jirani.
Akina mama walikuwa wanasafiri na kutembea umbali wa kilometa 21 kupata huduma za uzazi ama kujifungua kwa ngazi ya kituo cha Chita.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mkoa wa Morogoro utakimbizwa katika halmashauri zote tisa za Wilaya hadi Mei 14 ,2023, na kukabidhiwa wa mkoa wa Pwani Mei 15, 2023 .