Wananchi wampongeza Samia kuanza safari SGR
MOROGORO – WANANCHI wa Mkoa wa Morogoro na abiria waliosafi ri na treni ya mwendokasi (SGR) yenye namba E6800-01 kutoka Dar es Salaam – Morogoro ikiwa ni safari ya kwanza, wameguswa na mafanikio ya usafiri huo.
Wakizungumza na HabariLEO kwenye kituo cha abiria cha treni ya mwendokasi kilichopo Kihonda, Morogoro kwa nyakati tofauti walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuusimamia mradi huo na kuukamilisha na wao kuanza kunufaika.
Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam, Inda Mhando alisema alifika Morogoro kwa shughuli zake binafsi na baada ya kusikia kuanza kwa usafiri huo alishawishika kusafiri na treni hiyo wakati wa kurudi Dar es Salaam na watoto wake wawili wa kiume.
Costantine Makau alifurahishwa na huduma zinazotolewa za ukataji wa tiketi kwa mtandaoni kupitia moja ya benki na kupata tiketi yake mara moja kwa ajili ya safari kutoka Morogoro-Dar es Salaam.
Alisema alikata tiketi ya daraja la pili nauli ni Sh 21,500 kutoka Morogoro-Dar es Salaam.
SOMA: LATRA yatangaza bei Daraja la Kawaida SGR
Naye Mussa Khamis alisema usafiri huo ni mwepesi na mzuri kwa sababu una utulivu mkubwa na unaokoa muda.
“Ni usafiri rafiki katika shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma kwani tumetumia saa 1:30 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na huu ni muda mzuri kwa mfanyabiashara, mfanyakazi au mtu mwingine yeyote”.
Abiria mwingine Abubakar Daud alisema alipanda treni hiyo saa 12:30 asubuhi na kufika Morogoro Saa 1.56 asubuhi hiyo na kwamba usafiri huo upo vizuri na wa uhakika.