Wananchi wataka vifaa tiba zahanati Visakazi

WANANCHI wa kijiji cha Visakazi, kata ya Ubena, Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani wameiomba serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa watumishi, vifaa tiba na vitendea kazi katika zahanati ya kijiji hicho

Ombi hilo lilitolewa na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Jamila Makwaya wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya kijiji kwa kamati ya siasa ya Wilaya ya Bagamoyo katika mbio za Bendera ya chama Cha mapinduzi (CCM) zinazoendelea wilayani humo.

Alisema licha ya jengo la zahanati hiyo kukamilika kwa asilimia 100 bado kuna changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba, vitendeakazi pamoja na kukosekana kwa watumishi.

Advertisement

“Zahanati hii imekamilika tangu Julai mwaka jana mpaka sasa hatujapata vifaa tiba, jengo halina vitendea kazi na watumishi ikiwemo wauguzi hatuna tunaomba serikali itusaidie kutatua changamoto hiyo.”alisema

Alisema wananchi wamekuwa wakipata adha ya kwenda mbali kwa ajili ya matibabu hali ambayo imekuwa ikieendelea kuhatarisha afya za wananchi hususani wanawake wajawazito ba watoto.

Diwani wa kata ya Ubena, Geofrey Kamugisha, alisema zahanati hiyo imegharimu zaidi ya Sh milioni 67 ambapo Serikali Kuu imetoa milioni 53, wananchi Sh milioni 13 na Halmashauri ya Chalinze Sh milioni 10.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, wilaya ya Bagamoyo, Abdurashidi Zahoro, aliagiza Halmashauri ya hiyo kuhakikisha vifaa hivyo vinafika mapema.

“Naagiza vifaa ikifika mwezi wa nane viwe vimekuja hapa ili wananchi waendelee kupata huduma ya Afya kama ilivyokusudiwa na vifaa kama vinaletwa waangalie maeneo ya pembezoni kwanza”alisema

Mbali na hilo pia aliagiza Halmashauri ya hiyo kusaidia ujenzi wa zahanati ya Kijiji Cha Mwidu kutokana na kwamba wananchi tayari kwisha changia nguvu ambapo wametoa zaidi ya milioni 27.

5 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *