WAKUU wa mikoa wametakiwa kuhakikisha elimu ya kina inatolewa kwa wananchi juu ya haki, ulinzi, usalama na ustawi wa wazee.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wazee kata ya Mkonze, Mmkoani Dodoma kuelekea Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee inayofanyika Juni 15 kila mwaka.
Dk Gwajima amesema kutokana na kuboreshwa kwa huduma mbalimbali za kijamii nchini idadi ya wazee imeongezeka kutoka 2,507,568 hadi kufikia 5,008,339 ambayo ni sawa na asilimia 8.1 ya Watanzania 61,741,120.
Amesema serikali imeendelea kuadhimisha Siku ya kupinga Ukatili dhidi ya wazee Juni 15, ambapo maadhimisho hayo muhimu kwa ajili ya kuuhabarisha umma juu ya haki, ulinzi, maendeleo na ustawi wa wazee wetu.
“Ninachukua fursa hii pia kuwaomba Wakuu wa Mikoa yote nchini kuratibu maadhimisho haya kimikoa kwa kushirikiana na viongozi wa Mabaraza ya Wazee katika mikoa husika. Katika maadhimisho haya” amesema Waziri Dk Gwajima.
Waziri Gwajima ameendelea kusisitiza jamii yote kuacha kufanya ukatili kwa Wazee na makundi yote kwa ujumla na amewaomba wanahabari kutumia vyombo vyao kuelimisha na kuendelea kukemea masuala ya ukatili nchini kote.
“Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuwashughulikia ipasavyo wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya ukatili kwa makundi mbalimbali katika jamii hususani kwa wazee”. ameongeza Waziri Dk. Gwajima.
Maadhimisho ya Kupinga ukatili dhidi ya wazee mwaka huu yatafanyika katika ngazi ya mikoa kote nchini na kaulimbiu ni “Wazee Wanastahili Heshima na Usikivu Wetu”.