Wanaswa biashara ya mirungi, bangi Geita
WATU 67 wametiwa mbaroni na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya uingizaji, usafirishaji na usambazaji wa mirungi na bangi kwa kipindi cha mwaka 2023/24.
Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa, Martine Shigella amesema hayo katika mapokezi ya mwenge wa uhuru kutokea Kagera iliyofanyika shule ya Sekondari Bwongela wilayani Chato.
Shigella amesema huo ni mwendelezo wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambapo jeshi la polisi linaendelea kuhusisha makundi mbalimbali na kuunda kikosi kazi kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya.
Amesema watuhumiwa waliokamatwa kesi 51 zilifikishwa mahakamani huku kesi zingine bado zipo kwenye hatua mbalimbali ikiwemo kesi tatu zilizopo kwenye upelelezi.
SOMA: Bangi zamponza, ahukumiwa miaka 20
Amesema ndani kipindi cha mwaka 2023/24 misako imefanywa na jeshi la polisi na kufanikiwa kukamata bangi zenye uzito kilo 117 pamoja na mirungi kilo 120.
Ameongeza kuwa, huduma za dawati la uchunguzi na huduma za kisheria zimeendelea ndani ya kipindi cha mwaka 2023/24 ambapo mkoa umepokea jumla yall malalamiko 262 yaliyohusu rushwa na mengineyo.
“Kuna jumla ya kesi za watuhumiwa 22 na kesi ambazo zipo mahakamani ni sita ambazo zimeshamalizika na kesi zote serikali imeshinda kesi zote.
SOMA:Kilo 310 za bangi zateketezwa Arusha
“Aidha mapambano dhidi ya rushwa yameendelea kuhusisha elimu ya utoaji wa elimu, kwa njia za redio, mikutano ya hazara pamoja na kupitia viongozi wa dini.”
Akizungumza katika uzinduzi wa vilabu vya wapinga rushwa na madawa ya kulevya shule ya sekodari Runzewe, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava ameagiza vita ya dawa za kulevya iwe endelevu.
Amesema suala la uraibu wa madawa ya kulevya kwa sasa limegeukia vijana wadogo waliopo mashuleni ambapo ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kukemea ili kusaidia waweze kufikia ndoto zao.
Amesisitiza pia ajenda ya kukemea na kuichukia rushwa ianze kujengwa kwa watoto tangu wakiwa wadogo ili kuandaa mabalozi wa elimu hiyo na viongozi wa baadaye wazalendo na wapenda haki katika kutumikia taifa lao.