Wanawake 100,000 kuelimisha fursa za Tehama

TAASISI ya Wanawake 100,000 imepanga kuwafikia wanawake nchini na kuwaelimisha kuhusu fursa ambazo hawajazifikia hususani katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye utalii, lengo likiwa ni kukuza uchumi wao na nchi kwa ujumla.

Mshauri wa Masuala ya Utalii na Uchumi kutoka taasisi hiyo, Dk Theresa Mugodi alisema hayo Jumatatu Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi kuhusu kuwepo kwa kongamano lenye kuwakutanisha wanawake mbalimbali nchini litakalofanyika Oktoba 15, 2022.

Alisema kupitia kongamano hilo watawafikia wanawake walio wengi nchini kuweza kuelimishwa namna wanavyoweza kuzitumia fursa hizo za utalii wa ndani na kukuza uchumi na kutangaza utalii nchini.

“Tunataka kupitia wanawake, kampuni za simu nchini kuja na ujumbe mfupi wenye kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, hatua ambayo itawezesha wanawake kushiriki na kujielimisha pia,” alisema.

Alisema upo utalii wa maji chini ya bahari ambapo inatakiwa kuwepo picha za chini ya ardhi ambazo zitaongeza wigo wa watalii wanaoingia nchini lakini pia kuwasaidia wanawake kiuchumi.

Alisema kupitia kongamano hilo watabainisha ni fursa zipi wanawake wanaweza kuzifikia ikiwemo pia kupika chakula cha kiutamaduni kulingana na makabila yao, suala ambalo litavutia watalii kwa namna moja hadi nyingine.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Nangasu Warema alisema ipo haja ya kuelimishwa na ya kuwepo kwa uwiano wa fursa za kitalii kijinsia ili wanawake nao waweze kushiriki.

Alisema watahamasisha wanawake kujiunga katika makundi na wataomba benki nchini kusaidia wanawake wajasiriamali ili kuimarisha uchumi wao.

Alisema kupitia kongamano hilo, wanawake watahamasika na kuwezesha juhudi za serikali za kufikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025 na kuongeza mapato kufikia Sh bilioni sita.

Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Veronica Nicholas alisema kupitia kongamano hilo litasaidia wanawake kupambana na vitendo vya kikatili na kunyanyasika na kuvipunguza.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button