Wapanga kusaidia wanafunzi wenye uhitaji
Klabu ya Rotary Oyster bay Dar es salaam imepanga kuunga mkono miradi ya elimu kwa kusaidia wanafunzi wenye uhitaji kupitia mashindano ya mbio za mbuzi .
Shindano Hilo linatarajia kufanyika Septemba 7 mwaka huu katika viwanja vya The Green Oyster bay mkoani Dar es salaam, ambapo fedha zitakazopatikana zitaenda kusaidia kuboresha mazingira ya elimu, kutoa ufadhili kwa wanafunzi wenye uhitaji na kuimarisha miundombinu ya maji na usafi (WASH) mashuleni.
Akizungumza Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Vyombo vya Habari kutoka Vodacom, Bi Annette Kanora amesema kuwa wamejikita kwenye kutumia ubunifu wa aina mbalimbali ili kusaidia jamii katika shughuli za kimaendeleo na kijamii nchini kote, na baada ya kuona mafanikio yaliyopatikana katika mbio za mbuzi za mwaka 2023
“Tunaamini katika nguvu ya ushirikiano katika kutatua matatizo yanayoikabili jamii na kuleta maendeleo, hivyo tunawahisi wadau wengine wajitokeze na kuungana nasi katika kufanikisha mbio za mwaka huu na kutimiza lengo la kusaidia wanafunzi wenye uhitaji.” alisema Bi Kanora.
Rais wa Rotary Club of DSM Oyster Bay kwa mwaka 2024/25, Himanshu Bhattbhatt amebainisha kuwa mashindano ya mwaka huu yenye kaulimbiu ya ‘‘Carnival’’ yanaitambulisha zaidi Rotary na kukutanisha watu pamoja katika kuihudumia jamii.
“Kaulimbiu ya mwaka huu ni wito kwa wadau wote kukutana na kusherehekea ushirikiano wetu na mafanikio ambayo kwa pamoja tumeyapata katika kusaidia jamii. Kwa mara nyingine tena, tumejiandaa kuwa na siku iliyojaa furaha na shangwe kwa lengo la kusaidia jamii na hivyo tunawasihi watu wajitokeze kwa wingi,” alisema Bhattbhatt.