Wapinzani wa Yanga, Simba, Azam hawa hapa

CAIRO, MISRI; Mabingwa wa tanzania Yanga, wamepangwa kuvaana na Vital’O FC ya Burundi kwenye mchezo wa awali Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Yanga itaanzia ugenini. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Agosti 16-18 huku mkondo wa pili ukipigwa Agosti 23-25 mwaka huu.

Ikiwa Yanga itavuka hapo katika raundi ya kwanza itakutana na mshindi kati ya SC Villa Jogoo ya Uganda na Commercial Bank ya Ethiopia.

Michezo ya raundi ya kwanza itapigwa kati ya Septemba 13-15 huku michezo ya mkondo wa pili ikipigwa Septemba 20-22.

Advertisement

SOMA:https://habarileo.co.tz/yanga-yapewa-vitalo-azam-kuivaa-apr/

Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Azam FC wamepangwa kuvaana na APR FC ya Rwanda. Ikiwa Azam watapenya katika hatua hiyo watavaana na mshindi kati ya JKU ya Zanzibar na Pyramids ya Misri.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Tanzania, inawakilishwa pia na timu mbili ambapo mabingwa wa Kombe la Muungano Simba watamsubiri mshindi kati ya Uhamiaji ya Zanzibar na bingwa wa Kombe la Shirikisho nchini Libya, ili kukipiga kwenye mchezo wa hatua ya kwanza ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Coastal Union ya Tanga itaanzia hatua ya awali ambapo itakuwa na kibarua dhidi ya FC Bravos ya Angola na mshindi wa jumla kwenye mchezo huu atavaana na FC Lupopo ya DR Congo.