WAKAZI wa Kijiji cha Ruvumachini Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma, wameishukuru serikali kwa kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaomaliza kero ya muda mrefu ya maji safi na salama katika kijiji hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas, walisema, tangu serikali ilipoanza kujenga mradi huo, wana matumaini makubwa ya kuishi na kuwa na maisha bora na kuondokana na mateso makubwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji ya bomba.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Hagapi Komba, alisema, changamoto ya maji katika kijiji hicho ni kubwa na ya muda mrefu hali iliyosababisha baadhi ya watumishi wa serikali wanaopelekwa kufanya kazi, wakiwemo walimu wa shule ya msingi kuomba uhamisho kwenda shule nyingine na wengine kukimbia, ili kuepuka kero ya maji.

Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, Jonas Mbunda, alisema, uamuzi wa serikali kutoa kiasi cha Sh bilioni 1.3, kwa ajili ya kutekeleza mradi huo imethibitisha uaminifu wake kwa wananchi wa jimbo hilo na kudhihirisha kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Kanali Laban Thomas, ameuagiza Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Ruwasa), Mkoa wa Ruvuma, kuhakikisha inamsimamia mkandarasi anayejenga mradi huo, ili akamilishe kazi kwa wakati na ubora wa hali ya juu.
Pia amewataka amewataka wananchi wa kutunza mradi huo pamoja na vyanzo vya maji.