Wasaka dawa ukatili dhidi ya watoto

KUKITHIRI vitendo vya ukatili kwa watoto nchini, Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekutana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda kuweka mkakati wa kushirikiana kukomesha vitendo hivyo.

Akizungumza leo mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhili Magaya amesema ushirikiano kati ya jumuiya na wizara hizo itasaidia kudhibiti vitendo hivyo.

Amesema ukatili dhidi ya watoto na wanawake hujitokeza katika njia tofauti tofauti, inaweza kuwa kimwili, kingono au kifikra.

“Inaweza kufanyika mbele za watu, faraghani au mtandaoni na kutekelezwa na mpenzi au mtu mwingine yoyote. Bila kujali unafanyika vipi, wapi na umetekelezwa nani au ni kwa sababu gani? Ukatili  una madhara makubwa ya muda mfupi au muda mrefu,” amesema.

Amesema jumuiya hiyo  ya wazazi ina  wajibu wa kusimamia elimu,malezi,maadili na tamaduni kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba wameandaa  kongamano maalum la kitaifa la malezi litakalofanyika mapema mwaka huu.

Magaya amesema bado  mazungumzo  yanaendelea na wadau wengine, ili kuibua mjadala wa  kitaifa wa mmomonyoko wa maadili unaendelea kwa kasi kubwa hapa nchini na ukatili wa kijinsia na watoto unaoendelea.

Kikao hicho kimehudhuriwa na   Mwenyekiti wa wazazi Mkoa wa Dar es Salaam,  Khadija Ally Said ambae ndio mwenyeji wa kongamano hilo litakalozinduliwa  rasmi kitaifa mkoani Dar es Salaam.

Habari Zifananazo

Back to top button