Wasiokuwa na maadili kutengwa uchaguzi Pwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kimewaonya wanachama wake wanaotarajia kugombea nafasi za wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa mwaka 2024 kwamba kitawazingatia wale wenye maadili na wanaofuata sheria na kanuni za chama hicho.

Katibu wa siasa na uenezi wa chama hicho, mkoani Pwani, David Marandu alisema hayo katika hafla ya kupokea msaada wa fedha Sh milioni 5 za ujenzi wa ofisi ya CCM kata ya Picha ya ndege, wilayani Kibaha uliotolewa na mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo, Musa Mansour.

Alisema chama hicho katika uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo kitazingatia wanachama wenye maadili ambao wanafuata misingi na kanuni za chama na kwamba yoyote ambaye hatakuwa na sifa hizo hapaswi kuwa kiongozi katika jamii.

“Wakati tukijiandaa kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024 napenda kuwafahamisha kwamba ambaye hatakuwa na maadili na sifa nzuri ajue wazi jina halitarudi hivyo niwaombe muendelee kuzingatia maadili na kanuni za chama chetu.”alisema Mramba.

Aidha alisema wakati maandalizi ya uchaguzi huo yakiendelea ni vema wakaendelea kuwa wamoja na kushirikiana ikiwa ni pamoja na kukataa makundi ambayo yamekuwa yakiwagawa hatua ambayo itaisaidia chama kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo.

Akikabidhi msaada huo kwa Halmashauri Kuu ya Chama Cha mapinduzi ya kata hiyo, mjumbe wa kamati ya siasa Mkoa wa Pwani, Musa Mansour, alisema ametoa fedha hizo baada ya kugushwa na tatizo la kata hiyo la kutokuwa na ofisi.

“Msaada huu sio wa kwanza ninaendelea kutoa kwa ajili ya kujenga chama chetu na baada ya hili pia nitaenda hadi ngazi ya matawi kuhakikisha kwamba nasaidia kutoa vitegauchumi ambavyo vitawasaidia kiuchumi na sio kuwakumbuka nyakati za uchaguzi tu”alisema Mansour

Mwenyekiti wa CCM kata ya Picha ya Ndege, Grace Jungulu, alimshukuru mjumbe huyo kwa msaada huo ambapo awali walifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh milioni 4 kwa ajili ya ujenzi na kwamba bado msaada zaidi unahitajika kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button