Wasomi Afrika wakutana Dar kujadili uongozi

WASOMI, wadau na wataalamu kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Bara la Afrika wamekutana kujadili masuala yanayohusu uongozi na utawala bora.

Wamekutana Dar es Salaam kupitia kongamano la siku tatu la kimataifa kwa lengo la kuja na ushauri sahihi kwa serikali juu ya namna ya kuboresha maeneo yenye kasoro.

Kongamano hilo linalohusu masuala ya utawala, uongozi na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, liliandaliwa kwa ushirikiano wa vyuo vikuu vitatu; Chuo Kikuu cha Kabale (Uganda), Johannesburg (Afrika Kusini) na Chuo Kikuu cha Mzumbe cha mkoani Morogoro.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, Dk Ida Lyatonga ambaye ni Mhadhiri na Kaimu Amidi wa Shule ya Utawala na Uongozi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema lengo kubwa la kongamano hilo ni kujadiliana na kushauriana wanavyoweza kusaidia serikali za nchi zao kufanya maboresho ya kiutawala na uongozi kupitia utafiti wa wataalamu kutoka katika vyuo hivyo.

“Sote tunafahamu kwamba utawala ni eneo muhimu sana. Kongamano hili limeangazia maeneo kumi na nane ya kiutawala ikiwemo afya na uchumi, ambako tulipata wachangiaji kutoka zaidi ya nchi kumi za Afrika na wengine kwa njia mtandao kutoka Canada na Marekani,” alisema Dk Lyatonga.

Alisema nchi ambazo washiriki wake waliwasilisha utafiti wao ni pamoja na Afrika Kusini, Zimbabwe, Ghana, Uganda na Tanzania.

Alisema majadiliano hayo yamegusa maeneo ya uongozi na utawala kwenye vyuo, kwenye serikali za mitaa, serikali kuu na maeneo mengine ya taasisi binafsi ambayo yanahitaji kushauriwa ili kuboreshwa.

Profesa Josephat Itika wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema ili vyuo vikuu viweze kuzalisha viongozi bora ni lazima kazi hiyo ianzie kwenye ngazi ya familia na baadaye katika taasisi za elimu.

Kwa upande wake, Profesa kutoka shule ya uongozi, utawala na sera za umma wa Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini, Dominique Wizeyimana alisema ili kuwa na viongozi bora ni lazima kurithisha mbinu na ujuzi kutoka kwa kizazi kimoja kwenda kingine.

Alisema si rahisi vijana kupata ujuzi, uzoefu na kujiamini bila kupewa nafasi ya kujifunza, kufanya makosa na kujirekebisha. Alisema hawawezi kufanya hivyo bila kujifunza kutoka kwa waandamizi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x