Wataka umakini magari yanayosafirisha kemikali

Wataka umakini magari yanayosafirisha kemikali

KAMATI ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, imetaka tahadhari zianze kuchukuliwa dhidi ya ongezeko la magari yanayosafirisha gesi na kemikali za aina mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kupitia bandari au barabara.

Kamati hiyo iliyoketi leo chini ya Mwenyekiti wake, Salim Asas imesema kemikali hizo zinahusisha pia mafuta ya kuendeshea mitambo ikiwemo petrol na dizeli.

“Kuna haja kwa ofisi ya mkemia mkuu wa serikali ikaanza kutoa elimu kwa kamati za usalama barabarani nchini kote, ili nazo ziwe na maarifa ya kutosha ya namna ya kuwatahadharisha wananchi pindi majanga yanayohusiana na kemikali yanapotokea,” alisema Asas.

Advertisement

Asas alisema ongezeko la magari yanayosafirisha bidhaa hizo kwa matumizi ya viwandani na nyumbani kunatishia usalama wa watu na mali zao pale yanapoweza kupata ajali na hivyo ni lazima kuwe na mikakati ya wazi ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Katibu wa kamati hiyo, Mosi Ndozero ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa aliomba kikosi cha zimamoto kwa kushirikiana na hospitali wasaidie pia kuwaelimisha wananchi kuhusu aina ya vifaa vya kujikinga na matumizi yake wakati wa ajali na uokozi.

Wakati huo huo kamati hiyo imekitia nguvu kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa, ikikitaka kukazia matumizi ya sheria na elimu katika kukabiliana na makosa ya barabarani.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,  Alfred Mbena alisema wakati makosa ya barabarani yanayosababishwa na madereva wa bodaboda yakipungua, yale yanayosababishwa na bajaji yanazidi kuongezeka.

“Na kuna matukio ya uharifu yanayofanywa na madereva wa bajaji wanaopakia abiria hasa wa kike nyakati za usiku. Tunaendele kulifanyia suala hilo uchunguzi na tunaomba wanaokutana na changamoto wakati wakitumia usafiri huo watoe taarifa Polisi,” alisema.

Kamanda Mbena aliziomba mamlaka zinazotoa usajili wa bajaji kuangalia pia uwezekano wa kuweka ukomo wa idadi ya bajaji zinazotakiwa kufanya kazi katika kila mji ili kurahisisha udhibiti wake.

“Tusiendelee kutengeneza bomu ambalo hatujui lini litalipuka na litamlipukia nani. Kwanza madereva wengi wa vyombo hivi vya moto hawana elimu ya udereva na wanafanya kazi hiyo bila leseni, hiyo ni kwa sheria gani?” alisema.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Asas alisema kama kamati za usalama barabarani zimeundwa kwa mujibu wa sheria basi ni muhimu zikahakikisha sheria za usalama barabarani zinatumika ipasavyo na bila aibu ili kupunguza au kumaliza kabisa ajali zinazoepukika.

“Duniani kote mataifa yanayohesabika kuanguka ni yale yanayoshindwa kusimamia utekelezaji wa sheria zinazosimamia mambo mbalimbali. Kama kamati tunawatia moyo askari wetu wa usalama barabarani mtekeleze majukumu yenu kwa nguvu zenu zote na hakuna sababu ya kulegeza sheria,” Asas alisema.

Aidha kamati hiyo ilizungumzia pia namna ya kudhibiti magari yanayobeba abiria wanaokwenda minadani na matumizi ya wanyama kazi nyakati za usiku katika mkakati wake wa kupunguza ajali za barabarani.