MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA), imeeleza kuwepo kwa unafuu wa kodi kwa kila anayechangia mfuko wa elimu nchini kama ilivyoainishwa katika sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kupitia unafuu huo imeshauri wadau wa elimu na jamii kwa ujumla kuchangia katika elimu ili kuleta tija kwa taifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka kutoka TEA, Mwanahamisi Chambega amesema hayo mkoani Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari.
“Katika sehemu ya 12(1) imesema ukichangia kupitia mfuko huo utapata nafuu ya kodi lakini pia watu hao watakuwa kwenye kanzi data ya mfuko wa elimu ya taifa kwa hiyo wataendelea kutambuliwa na taarifa zao kuwekwa kule na watafahamika na watu wote,” amesema.
Ametaja faida nyingine kwa mchangiaji katika elimu ni kupata hati ya utambuzi.
“Tunahamasisha na wengine mmoja mmoja kuchangia kupitia taasisi hiyo kwa kuwa ukichangia kupitia mfuko wa elimu Tanzania kuna faida.
“Tunaendelea kuhamasisha ili watu wachangie waweze kupata faida hizo ambazo zinatokana na sheria ya TEA na sheria ya kodi ambayo imeanzishwa na bunge.
“Kwa sasa mwitikio ya wadau siwezi kusema ni mkubwa sana au ni mdogo yaani umekuwa ni hafifu lakini sio sana wadau wengi wanachangia lakini hawapitii mfuko wa elimu wanachangia wenyewe wenyewe ile ya kwamba wanakosa kutambuliwa kihalali,” amesema.
Amesema wadau hao ambao hawapitii kwenye mfuko huo katika jamii wanatambuliwa na wachache, lakini pia wanaonekana ni hafifu katika uchangiaji wao.
“Tunawahamasisha waongeze zaidi katika kuchangia kupitia mfuko huo kwa kuwa ni wa taifa ambao umeanzishwa na sheria ya nchi ya bunge,” amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka mamlaka hiyo, Masozi Nyirenda alisema mfuko huo ulianzishwa kwa sheria na 8 ya mwaka 2001 na sheria ya bunge katika sheria hiyo hiyo ilianzisha Mamlaka ambayo inasimamia mfuko huo.
Comments are closed.