Wataka waliotajwa ripoti ya CAG washughulikiwe

SHIRIKA la HakiElimu limeitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya wahusika wote waliotajwa kwenye ubadhirifu uliobainishwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya mwaka 2021/2022.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage akizungumza leo Mei 9, 2023 jijini Dar es Salaam amesema licha ya serikali kuboresha mazingira ya elimu, lakini kuna changamoto kubwa ambazo zingeweza kutatuliwa na fedha ambazo zimetapanywa na baadhi ya taasisi na mashirika ya umma kama ilivyobainishwa kwenye ripoti ya CAG na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 813.5.

Dk Kalage amesema iwapo fedha za Covid-19, Wizara ya Elimu ilipata mgao wa Sh bilioni 300 na ikafanikiwa kujenga madarasa 12,000 katika shule za sekondari, vituo shikizi 3,000 na mabweni 50 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, sh bilioni 813.5 zingedhibitiwa zingeweza kujenga miundombinu ya sekta ya elimu zaidi ya mara mbili ya miundombinu iliyojengwa kwa fedha za Covid 19 na ingepunguza changamoto za sekta ya elimu.

“Watu wanatapanya pesa, wanafanya ubadhirifu na wapo mtaani wanadunda hawachukuliwi hatua yoyote, ndio maana kila anayepewa fursa anaona ni mahali pa yeye kula,” amesema Dk Kalage na kuongeza:“Pamoja na jitihada za serikali kufungua nchi, mama kwenda huko na kule kuomba misaada na mikopo, lakini pesa zinaingizwa kwenye mifuko iliyotoboka, sehemu kubwa watendaji hawazifanyii kazi zilizokusudiwa, tutawabebesha watoto na wajukuu zetu mzigo wa madeni makubwa miaka ya baadae.

“Na hii inakuja kwa vile hatuna vipaumbele, kila kiongozi anayeingia madarakanai anaingia na vipaumbele vyake bila kujali alivyoviacha mwenzake, tumekuwa tukitapanya rasilimali za nchi hii kwa kutowekeza kwenye kipaumbe kimoja, mfano Korea wamefanikiwa kwa ajili kuna sera madhubuti kiongozi yoyote anayeingia kipaumbele anachokikuta anaenda nacho mpaka mwisho.

“Na hapa iwe hivyo, kuwe na sera itakayomlazimisha kiongozi yoyote atakaeingia asimamie kipaumbele kilichopo mpaka mwisho tunafanya tathmini kama kimefanikiwa au la, na kama hakijafanikiwa kwa nini?

“Kunakuwa na tathmini ya kina…Wizara ya elimu kwa miaka mitano imekuwa ikitengewa bajeti ndogo isiyokidhi wakati pesa nyingi zinatapanywa kama ilivyooneshwa kwenye ripoti ya CAG,”amesema.

Akichambua ripoti ya CAG, Dk Kalage anasema ripoti hiyo inaonesha ipo mianya mingi ya matumizi mabaya ya fedha za umma na udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na kwamba changamoto hizo zingeweza kushughulikiwa ipasavyo, fedha nyingi zingeweza kuokolewa na kuelekezwa katika maendeleo ya Taifa ikiwemo utatuzi wa changamoto za sekta ya elimu.

“Mathalani kwa mujibu wa ripoti ya CAG 2021/2022 sh bilioni 88.42 zilizotolewa kama mikopo kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mamlaka za serikali za mitaa 180 hazikurejeshwa, mamlaka 98 hazikuwasilisha kiasi cha sh biloni 15.9 zilizokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato na Sh bilioni 8.99 zilikopeshwa na halmashauri lakini hazikurejeshwa.

Ripoti hiyo ya CAG inaonesha pia mamlaka za serikali za mitaa kushindwa kukusanya Sh bilioni 76.56 walizotakiwa kukusanya kutokana na mapato ya vizimba, tozo, ushuru na leseni.

Amesema ripoti inaonesha ubadhirifu katika baadhi ya miradi mikubwa mfano Shirika la Reli nchini (TRC) lilisababisha hasara ya sh bilioni 503.2 kwa kumkataa mzabuni aliyetaka kulipwa Sh bilioni 616.4 na kumpa kazi mzabuni wa Sh trilioni 1.119 sawa na ongezeko la asilimia 82 isiyokuwa na ulazima.

Pia amefafanua kuwa ripoti ya CAG imeonesha Shilingi milioni 632 za mradi wa EP4R zilipotea katika ujenzi wa chuo kipya cha uwalimu Sumbawanga chenye kugharimu sh bilioni 3. Ripoti pia inaonesha zaidi ya sh bilioni 50 zilitumika kununua vifaa tiba hewa katika sekta ya afya.

“Taarifa hiyo ya CAG pia inabainisha ubadhirifu katika Wizara ya Ujenzi ambayo haikukusanya sh bilioni 41.4 iliyotakiwa kutozwa wakati wa kusafirisha mizigo mizito, huku wakala wa Majengo (TBA) na Mahakama pia hazikutoza sh bilioni 8.43 wakati wa kutoa hduma kama zinavyopaswa.

Ripoti pia inabainisha Taassi za Serikali Kuu zilitumia Sh bilioni 3.39 huku Mamalaka za serikali za Mitaa zikitumia sh bilioni 26.28 kununua magari hewa,” amesema na kuongeza:“Maeneo haya machache ya taarifa ya CAG yanaonesha zaidi ya Sh bilioni 813.5 zimepotea, ikiwa serikali imetumia Sh bilioni 353.4 fedha za mgao wa mapambano dhidi ya Covid- 19 yaliweza kujenga madarasa 12,000 katika shule za sekondari, vituo shikizi 3,000 na mabweni 50 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, Sh bilioni 813.5 zingedhibitiwa zingeweza kujenga miundombinu ya sekta ya elimu zaidi ya mara mbili ya miundombinu iliyojengwa kwa fedha za Covid 19.”

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x