MRAJISI na Mtendaji Mkuu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dk Benson Ndiege amewataka wakulima kuhakikisha wanapopeleka mizigo yao kwa ajili ya kupima kufanya hivyo kupitia mizani ya kidijitali ili kuepuka kupunjwa mazao yao.
Dk Benson amezungumza hayo mbele ya waandishi wa habari kuelekea ufunguzi wa kiwanda cha kubangua korosho kinachosimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mkoa wa Mtwara.
SOMA: ‘Kufikia 2030 korosho ibanguliwe nchini’ …
Amesema baadhi ya Vyama vya Ushirika (AMCOS) na watendaji wa vyama hivyo hawataki kutumia mizani hizo na wanaziharibu ili zisifanye kazi kama inavyotakiwa ili kuendelea kumpunja mkulima hivyo amewataka viongozi hao wa Amcos na vyama vikuu vya ushirika kuhakikisha mizani hizo zinatumika kwani zimekuja kwa ajili ya kumlinda mkulima.
“Utumiaji wa mizani hizo unalengo la kuongeza uwazi na kumlinda mkulima ili aweze kupata fedha kulingana na kazi aliyoifanya hivyo mkulima anapokwenda kupima taarifa za mzigo wake zinawafikia wahusika ikiwemo mkulima mwenyewe,”amesema Dk Benson.
SOMA: Rais Samia aipaisha korosho Afrika
Kuelekea msimu wa korosho ambao minada inakwenda kuanza rasmi Oktoba 11,2024, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred amewaomba wanunuzi kutoa bei nzuri itayokuwa na manufaa makubwa kwa wakulima kuwa na ustawi wa kuhudumia zao hilo.
“Tutasimamia zaidi kwenye upande wa waendesha ghala kuhakikisha kwamba wanazingatia maelekezo ambae ataenda kinyume cha utaratibu kutozingatia taratibu za zao kuhakikisha zao tunalolipata linakuwa zuri”amesema Francis