Watakiwa kurahisisha huduma kwa walemavu
WADAU mbalimbali wanaotumia huduma zitokanazo na teknolojia wameomba taasisi za fedha nchini, kurahisisha huduma hizo kwa watu wenye ulemavu wakiwemo wa macho.
Ombi hilo limetolewa jijini Arusha katika mkutano wa Asasi za Kiraia (AZAKI) na wadau hao ambapo walitoa Rai kwa taasisi hizo, kuwapatia mfumo shirikishi, utakaowasaidia kwenye utumiaji wa teknolojia kwenye maeneo mbalimbali.
Renatusi Rupoli ambaye ni mlemavu wa macho kutoka mkoani Iringa, amesema watu wasioona huwa wanatumia mitandao kwa njia ya sauti, ambapo alihoji kwa nini kusiwepo na ‘Software’ kama hizo ambazo zinajumlishwa kwenye mashine za kutolea fedha (ATM) katika benki, ili kupunguza usumbufu wakutafuta wasaidizi wakati wa kutumia huduma hizo.
“Katika simu na kompyuta kwa sasa hatuombi msaada wa mtu,sababu kuna software zinazotusaidia kutumia bila msaada wa mtu tofauti na mashine za ATM, tunaomba angalieni jinsi ya kutusaidia ili tusitegemee watu kuingia nao kutusaidia katika ATM,”.
Akijibu hilo katika mkutano huo, Mkuu wa Mauzo Kitengo Cha Masoko ya Nje kutoka Benki ya Stanbic, Amal Baziad amesema wamechukua ombwe hilo na kuona jinsi gani watalifanyia kazi ili kupata ufumbuzi.
“Ninaimani kuwa siyo tu Stanbic pekee ambao hatuna huduma hii ya kuwasaidia walemavu kutoa fedha ATM bila msaada wa mtu,lakini naichukua kama changamoto na tuone namna gani tunaifanyia kazi, ili kuwawezesha wateja wetu kupata huduma rafiki kwao.”
Pia Baziad ameshauri kuwepo kwa huduma rafiki kwa wazee na wananchi waishio vijijini, kwa kuwawezesha kufungua akaunti benki, kwa kutumia mitandao badala ya kufuata huduma hizo, kwa mawakala wa benki ambao mara nyingi hupatikana mijini.