Watakiwa kutenga maeneo ya wafugaji

Mifugo inatakiwa kutengewa maeneo maalumu.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amezitaka halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji, ili kukuza sekta hiyo na kuepusha migogoro ya matumizi bora ya ardhi.

Waziri Ndaki amebainisha hayo katika  ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji katika vijiji vya Tanga na Njiwa.

Amesema serikali ina nia nzuri ya kuendeleza sekta ya mifugo na kuzitaka halmashauri hizo na mamlaka za serikali za mikoa kutekeleza agizo hilo.

Advertisement

Pia amewataka wafugaji kutolisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

Amesema serikali imeelekeza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kuanzia ngazi ya kijiji, ambayo hayajasajiliwa, yanatakiwa kutambuliwa rasmi na kusajiliwa pamoja na kulindwa na kuhakikisha yanatumika kama ilivyopangwa kwa ajili ya kulishia mifugo pekee pamoja na kuwataka wafugaji kutoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi na mapori tengefu.