Watakiwa kutunza miche kuleta matokeo chanya

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (wa pili kulia), akikagua kitalu cha miche.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, amekagua mradi wa kitalu cha miche ya miti wenye thamani ya Sh milioni 43, unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Akizungumza leo katika ziara, Masanja amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuitunza miche ya miti watakayokabidhiwa na TFS, ili iweze kuleta matokeo chanya ya kuhifadhi mazingira.

“Tuwaombe wananchi, miche hii watakapogawiwa waitunze vizuri kwa ajili ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo,” alisema Naibu Waziri.

Advertisement

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo, awamu ya kwanza zimetolewa fedha kiasi cha Sh milioni 17  kwa TFS, ambapo serikali itaendelea kutoa fedha kwa awamu nyingine, ili kukamilisha mradi.

Amesema lengo la uanzishwaji wa kitalu hicho ni kupunguza athari za uharibifu wa mazingira, hususan katika Mkoa wa Mwanza, ambapo kwa sasa utekelezaji wake umeanzia Wilaya ya Magu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali amesema kupitia kitalu hicho wananchi wa Wilaya ya Magu watanufaika sana, kwa sababu miche itapelekwa kwenye maeneo ambayo yalikwishaharibika, ili kuyarudisha kwenye asili yake ya awali na kutoa rai kwa wananchi kuitunza na kuilinda miche ya miti watakayokabidhiwa.

“Kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake na kwa wale wafugaji msiingize mifugo kwenye maeneo ambayo tumepanda miti,”amesema.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa TFS, Kanda ya Ziwa, Thomas Moshi, amesema kitalu hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha miche 300,000 kwa mwaka, hivyo kuendelea kuihudumia jamii ili kuhakikisha maeneo ambayo hayana miti uoto wa asili unarudi.