Watakiwa wasiwageuze mtaji waliomaliza la saba

WAZAZI na walezi wenye watoto waliohitimu darasa la saba Wilaya Mpanda,  mkoani Katavi wametakiwa wasiwageuze watoto wao mtaji wa kujiingizia kipato, hali inayosababisha baadhi kujiingiza kwenye vitendo visivyo na maadili na wengine kuozwa wakiwa wadogo.

Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Mpanda Method Mtepa, alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe za mahafali ya darasa la saba shule ya Msingi Nyerere, iliyopo mjini Mpanda.

“Imefikia hatua baba au mama anamuuliza mtoto wa kike, kwa hiyo leo mwanangu hatuli? Unategemea huyu mtoto wa kike akupe nini? Anafanya kazi gani?” Alihoji na kuongeza:

“Acheni kuwategemea watoto wa kiume kwa kuwafanyisha kazi za ajabu, ili muweze kukidhi nafsi za maisha yenu, hatimaye mtoto wa kike atajiingiza kwenye vitendo vya ngono na wakiume atajiingiza kwenye mapenzi ya jinsia moja,” alisema.

Aliwataka wazazi na walezi kuwajibika katika majukumu yao, ikiwemo kuwapatia watoto haki za msingi ikiwemo kuwahudumia chakula, malazi na mavazi.

Wanafunzi waliohitimu darasa la saba katika shule hiyo ni 326, ambapo wasichana ni 146 na wavulana 180, huku 43 walishindwa kuhitimu darasa hilo kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo utoro, mimba na mmoja kufariki.

 

Habari Zifananazo

Back to top button