BALOZI wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Ali Jabir Mwadini amesema zaidi ya Watanzania 900 mwaka huu wamepata fursa ya kwenda kufanya kazi nchini humo kupitia utaratibu rasmi wa ajira.
Ametoa kauli hiyo jana mjini Riyadh wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Tanzania kwenye mkutano ulioendeshwa kwa njia ya mtandao, kuzungumzia fursa mbalimbali zilizopo huko na jinsi ya kuzichangamkia.
“Hivi juzi tu kampuni kubwa ya Saudi Arabia ya Almarai ilikuja nchini Tanzania kufanya interview (usaili) wa nafasi za kazi kwa Watanzania, walishirikiana na kampuni ya Mtemvu ambaye ni Mtanzania. Walipata Watanzania zaidi ya 500 kutoka Bara na wengine zaidi ya 400 kutoka Zanzibar waliochaguliwa kuwa wamefaa kwenda kufanya kazi Saudi Arabia, hivyo fursa za ajira huku zipo,” alisema Balozi Mwadini.
Alisema mbali ya ajira hizo 900 mpya, wapo Watanzania 1,200 wanaofanya kazi Saudia kwa sasa na wanafanya kazi kwa mikataba rasmi inayotambulika na serikali.
Alieleza kuwa ofisi ya ubalozi ina mawasiliano nao ambapo ikitokea changamoto, wanatoa taarifa kwenye kundi la Watanzania na hatua kuchukuliwa.
Alizitaja fursa za kazi zilizopo Saudi Arabia ni udereva, uhudumu wa hoteli na migahawa, uuguzi, watoa huduma za afya na fani nyingine za utaalamu, na kuwataka Watanzania wanaotaka kufanya kazi huko wafuate taratibu rasmi ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kwa kutumia njia ya panya.
Fursa nyingine Balozi Mwadini aliyotaja ni elimu na kusema kila mwaka Saudi Arabia hutenga nafasi 160 za ufadhili wa masomo kwa Watanzania kwenda kusoma nchini humo taaluma mbalimbali na kuwataka vijana kuzichangamkia kwa sababu pamoja na fursa hizo kutolewa, bado nafasi zinabaki kwa kukosa wahitaji.
“Nimezungumza na Waziri wa Elimu wa Saudi Arabia, kaniambia kila mwaka wanatenga nafasi 160 za fursa ya masomo kwa ajili ya Watanzania, lakini ni bahati mbaya vijana wetu hawazichangamkii, zinabaki, nitoe mwito kwa wanaopenda kuja kusoma hapa ombeni hizo fursa,” alisema Balozi Mwadini.
Alisema baadhi ya wananchi wanadhani kuwa kwenda kusoma Saudi Arabia ni kusoma Lugha ya Kiarabu pekee, akisema mawazo hayo si sahihi.
Alifafanua kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi zenye vyuo bora duniani vinavyotoa taaluma katika fani mbalimbali kama udaktari, uhandisi, biashara, teknolojia ya habari na kompyuta na nyinginezo.
Alisema ubalozi unaangalia jinsi ya kufanya ili kuandaa mkutano wa siku moja kuelimisha fursa zilizopo Saudi Arabia ili Watanzania wazichangamkie.
Akizungumzia biashara, alisema kuna masoko ya bidhaa za samaki, nyama, juisi na kufafanua kuwa soko la nyama kutoka Tanzania limefunguliwa rasmi tena Juni mwaka huu baada ya kufungwa kwa miaka 20 kutokana na mifugo kushambuliwa na magonjwa ya midomo na miguu.
Comments are closed.