Watanzania sasa kuwekeza kidigitali

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Mtandao wa Simu wa Vodacom kwa kushirikiana na Kampuni ya Bima na Uwekezaji ya Sanlam wamekuja na fursa ya kuwezesha watanzania kufanya uwekezaji kidijitali kupitia M-Wekeza inayomuwezesha mwananchi wa kawaida kuwekeza kuanzia kiwango cha chini Sh 1,000 na kuendelea

Hayo yameelezwa wakati wakifanya mazungumzo kupitia Voda chat iliyofanyika katika mitandao ya kijamii ya Facebook pamoja na X wakizungumzia mifumo mbalimbali ya uwekezaji ya pamoja ikiwemo mfumo wa uwekezaji kidijitali.

Awali, Mkurugenzi wa M-pesa, Epimack Mbeteni alisema walianza kwa huduma za kifedha ambazo ni za kawaida zinazowezesha watu kutuma na kupokea fedha na wakaona umuhimu wa kutumia misingi hiyo kuwezesha kutoa huduma nyingine kwa msaada wa teknolojia ili kusukuma ajenda za kiuchumi.

Mbeteni alisema Kupitia teknolojia wameweza kuleta huduma kama M-Wekeza kwa kushirikiana na Sanlam ambayo inamsaidia na kumuwezesha mtanzania kufanya uwekezaji kuanzia kiasi cha Sh 1,000 na kuendelea pia huduma nyingine walizoweza kufanya wao kama Vodacom ni bima, upatikanaji wa mikopo kupitia M-pawa, Songesha.

Akifafanua juu ya uwekezaji huo Mbeteni alisema huduma hiyo imeanzishwa kwa ajili ya kusaidia wananchi kuwekeza na kuzalisha fedha zao kwa urahisi na kuweza kufaidika na faida nyingi kutokana na huduma hiyo ikiwemo riba ya asilimia 13 ambayo inazaa kila siku baada ya kufanya uwekezaji.

Mbeteni alisema wameshirikiana na Sanlam kwa sababu ni mona ya kampuni kubwa katika ukanda wa jangwa la Sahara na Afrika na wanauzoefu zaidi ya miaka 25 na kufanya uwekezaji na wanaendelea na ubunifu mwingine unaokuja ili kubadilisha maisha ya watanzania.

Katika hatua nyingine Mtaalamu wa Uwekezaji, Edmund Munyagi alisema amekuwa katika sekta ya uwekezaji kwa muda na alianza kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja kwa takriban miaka saba hadi nane na haijawahi kutokea huduma bora kwa wawekezaji kama M-Wekeza.

Akifafanua hali ilivyokuwa hapo awali Munyagi alisema waliokuwa wakiwa wanafaka kufungua akaunti za uwekezaji walikuwa wanatakiwa kujaza makaratasi na kuyapeleka sehemu ili akaunti iweze kufunguliwa na inapotokea wakihitaji fedha walitakiwa kujaza tena na kusubiri kwa siku kadhaa kitendo ambacho ilikuwa ni ngumu iwapo unahitaji wa haraka na fedha.

Alisema kwa sasa mambo ni tofauti kwani mtu anaweza kuwekeza kupitia simu ya mkononi na kama unatumia simu ya Vodacom ni rahisi zaidi kwani wanakuwa na taarifa zako tayari wamezihifadhi, hivyo hakuna haja ya kujaza barua za serikali za mitaa na taarifa nyingine.

Pia inampa nafasi mtanzania kuwekeza kwa kutumia mtaji mdogo kwani huduma ya M-Wekeza inampa mtu nafasi ya kuweza hata kwa kuanza na kiasi cha Sh 1,000 na kuongeza kuwa kupiti huduma za uwekezaji zinakuja na elimu ambayo inawezesha watu kujifunza kuhusu uwekezaji.

“Watu wamekuwa na dhana potofu ya kudhani kwamba ili mtu aweze kufanya uwekezaji anahitaji kuwa na fedha nyingi kitu ambacho sio kweli kwani ukiwa na kiwango kidogo na ukawekeza inakusaidia kujenga tabia na nidhamu kwa sababu ukiweza kukibana kiwango kidogo kitaongezeka zaidi,” alisema Munyagi.

Mapinduzi ya kidijitali au tehnolojia inarahisisha zaidi kwa mtu kuweza kuwekeza ili waweze kupata manufaa kwenye maisha yao na elimu inapokuwa inatolewa katika majukwaa tofauti inaenda kuwapa watu faida zaidi katika uwekezaji wao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button