Watanzania watakiwa kupunguza unywaji wa Pombe

DAR ES SALAAM: Watanzania wametakiwa kupunguza unywaji wa pombe ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambaye amesema sababu kubwa ya kuongezeka kwa magonjwa hayo ni matumizi makubwa ya unywaji pombe.

“Takwimu zinaonesha Tanzania ni nchi ya tatu kwa matumizi ya pombe barani Afrika ikiongozwa na Uganda.”Amesema na kuongeza

“Hatusemi msinywe pombe, lakini tunasema mpunguze unywaji wa pombe kupita kiasi, takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha Tanzania Watu kuanzia umri wa miaka 15 na kuendelea kwa mwaka tunakunywa Lita 10.4 za pombe.” Amesema na kuongeza

“Kiasi hichi cha pombe kinachonywewa nchi nzima, kikagawanywa kwa idadi ya Watanzania miaka 15 na kuendelea, ni sawasawa tunatandika kwa mwezi Lita 1 kwa mwaka Lita 10.4, tupo nafasi ya tatu Afrika, baada ya Uganda anafuata Shelisheli halafu sisi.

“Prof. Mohamed Janabi (Mkurugenzi wa Muhimbili) anasemaga bia moja mbili ukimaliza unaangalia mpira wako unaondoka, sio uweke mzigo wa bia hapana,”amesema.

Ummy ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akizindua kampeni ya kuelimisha jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo katika hatua nyingine amesema ugonjwa wa Saratani umeongezeka kwa kasi mwaka 2020 ambapo umeonesha vifo vipya zaidi ya 40,000 ukiongozwa na Saratani ya Mlango wa Kizazi.

“Tusipochukua tahadhari ugonjwa wa saratani unaweza kufikia vifo milioni moja ifikapo 2050, Saratani inachangia kwa asilimia 33 ya vifo vyote nchini Tanzania,”ametahadharisha Ummy.

Habari Zifananazo

Back to top button