watendaji vituo vya kura washauriwa kupitia sheria

MTWARA: WATENDAJI wa vituo vya kupigia kura katika Jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara wametakiwa kusoma kwa umakini katiba, sheria na kanuni wakati wa utekelezaji wa majukumu hayo.

Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 26, katika mafunzo ya siku mbili yaliyohusisha na kiapo cha kujitoa uwanachama na kutunza siri kwa watendaji hao wa vituo hivyo yaliyofanyika kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani humo kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Akifungua mafunzo hayo, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Tandahimba Ramadhani Mmbughu amesema mafunzo hayo yamehusisha watendaji hao 1771 wakiwemo wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo wataofanya shughuli za uchaguzi katika vituo 569 vilivyopo kwenye kata 32 za halmashauri hiyo.

Aidha mafunzo hayo yana lengo la kubadilishana uzoefu na kujadiliana namna ya kufanikisha uchaguzi huo katika maeneo yao pia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua mbalimbali za zoezi hilo la kupiga na kuhesabu kura.

“Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na sheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa hasa katika ngazi ya kituo,”amesema Mmbughu

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwaasa watendaji hao kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi ila wasiache kusoma katiba, sheria na kanuni zinazotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

“Someni kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume na ulizeni ili mpate kufafanuliwa kwenye maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine pengine yatakuwa na changamoto za kufahamu,”amesisitiza Mmbughu

Sambamba na hilo miongoni mwa majukumu na wajibu wa watendaji hao wakati wa zoezi hilo ikiwemo kuzingatia muda wa kuripoti eneo la kituo cha kupigia kura ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima wakati wa zoezi hilo na mengine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button