DAR ES SALAAM: MRATIBU wa Kitaifa wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema kuwa licha ya nchi kutambua mchango wa wanawake katika utetezi wa haki za binadamu, lakini wengi wao wameingia kwenye harakati hizo kwa ajili ya ajira badala ya kufanya kazi hiyo kwa wito kama inavyotakiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Olengurumwa amewataja wanawake kama Getrude Mongela, Mary Lusimbi, na Anna Tibaijuka kuwa ni miongoni mwa wanawake waliokuwa na moyo wa dhati wa kujitoa kwa ajili ya kutetea haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Olengurumwa, watetezi wa haki za binadamu wa kizazi cha sasa, hasa wanawake, wanakosa uvumilivu katika kazi na pia hawashirikiani kama ilivyokuwa kwa wanawake wa zamani. Amesema kuwa awali, wanawake walikuwa wakikutana na kujadili ajenda za kitaifa kwa pamoja, lakini sasa kila mmoja anafanya kazi kivyake.
“Watetezi wa sasa wanachukulia utetezi kama ajira. Hawana uvumilivu na kila mmoja anapambana kivyake. Anayetetea haki za watoto ana lake, anayetetea haki za wanawake naye ana lake. Zamani, mama zetu walijadili kwa pamoja masuala ya mwanamke, mtoto, demokrasia, ardhi na uchumi, jambo lililosaidia kuimarisha utetezi wa haki,” amesema Wakili Olengurumwa.
SOMA ZAIDI: Mtandao wa Wanawake watoa msukumo kwa nafasi za uongozi
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Olengurumwa amesema kuwa wanawake walikuwa na mchango mkubwa katika harakati za uhuru wa Tanzania. Amewataja wanawake kama Bibi Titi Mohamed walimsaidia Mwalimu Julius Nyerere kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhuru wa nchi bila vita.
“Wanawake waliongoza harakati za ukombozi wa taifa letu. kwa mfano, Bibi Titi aliongoza mikutano ya hamasa akishirikiana na Mwalimu Nyerere ili kuwaelewesha wananchi umuhimu wa uhuru. Hata hivyo, historia haijatilia mkazo mchango wa wanawake katika kutetea haki za binadamu,” amesema.
Olengurumwa amesisitiza kuwa ikiwa wanawake watapewa nafasi zinazozuiwa na mifumo na historia, wanaweza kuwa wadau wakubwa wa maendeleo ya taifa. Aliutolea mfano Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995, ambapo wanawake wengi wa Tanzania walishiriki na kutoa maazimio 12 ya kutetea haki za binadamu, hasa za wanawake.
Aidha, Olengurumwa ametoa wito kwa watetezi wa haki za binadamu, hususan wanawake, kurudi katika misingi ya mshikamano badala ya kufanya kazi kwa maslahi binafsi.
“Watetezi wa haki za binadamu wanapaswa kufanya kazi kwa umoja na si kwa maslahi binafsi. Ikiwa mtu anatafuta ajira na mshahara mzuri, basi afanye kazi benki au kwenye sekta nyingine,” amesema Olengurumwa.