Watoa elimu kuepusha udumavu kwa watoto

WAHUDUMU wa afya ngazi ya jamii (WAJA) kata ya Mwendakulima Manispaa ya Shinyanga wameonesha kwa vitendo mbele ya wazazi namna ya upikaji uji wa virutubisho kwa watoto ili kuwaepusha na udumavu.

Wahudumu wa afya ambao ni Rehema Juma na Emanuel Malale wametoa elimu hiyo kwa nyakati tofauti tarehe 4,Oktoba,2024 katika Maadhimisho ya Afya na Lishe katika kata ya Mwendakulima.

Rehema Juma amesema unga wa Lishe hautakiwi kuchanganywa nafaka zingine kama karanga kwani hutengeneza sumu kavu unapokaa muda mrefu kinachotakiwa unga huo usikobolewe na uchanganywe ukiwa tayari jikoni.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Mwendakulima Leonora David amesema mjamzito, mtoto mwenye umri wa kuanzia miezi sita hadi miaka mitano wanatakiwa wapatiwe mlo wenye virutubisho mwilini.

David amesema wajawazito wanatakiwa wapatiwe vyakula bora ili kujenga afya ya mtoto akiwa bado tumboni ndiyo maana elimu hii ya lishe imekuwa ikitolewa kliniki kila wahudhuriapo.

SOMA: Majaliwa kufunga mkutano wadau wa lishe

David amesema wapo wajawazito ambao wamekuwa wakihudhuria kliniki mimba imefikisha umri wa miezi sita au nane ndiyo anafanya hudhurio la kwanza hiyo haitakiwi utaratibu uliopo kujua maendeleo ya awali ya mtoto hivi sasa Mahudhurio yanatakiwa manane na yote yatimizwe.

“Tukitaka kuondoa udumavu kwa watoto wetu tutumie makundi matano ya vyakula na leo elimu iliyotolewa namna ya upikaji uji ndiyo tukaifanye majumbani mwetu tunapowaandalia watoto”amesema David.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Dk Fredrick Malunde ambaye ni bingwa wa magonjwa kwa njia ya mionzi amesema ukiwa na Mjamzito na mtoto mwenye afya bora utakuwa na changamoto ndogo ya kutoa fedha nyingi kwaajili ya kumuhudumia hospitalini.

SOMA: Dkt. Dugange: Toeni fedha za afua za lishe

Dk Malunde amesema ukiacha kufuata ushauri wa wataalamu ndiyo utatumia gharama kubwa kwenye masuala ya afya.

Habari Zifananazo

Back to top button