Wavuvi watakiwa kutumia fursa za mikopo

DODOMA; WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema fursa za kukopa zipo, hivyo wajasiriamali wakiwemo wavuvi wazitumie.
Ametoa kauli hiyo leo bungeni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nungwi, Simai Hassan Sadick aliyehoji mikakati ya serikali kuhusu mikopo kwa wavuvi.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema sekta ya uvuvi imewekwa kwenye sera ya uchumi wa buluu na serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar, hivyo kuwataka wanaotaka kuingia kwenye sekta hiyo na wale ambao tayari wapo huko watambue serikali inalitambue eneo hilo.
“Suala la mikopo nataka niwape faraja wale wote walioanza, wanaotaka kuanza kuingia kwenye sekta ya uvuvi, serikali imezungumza na taasisi za fedha kwa maana ya mabenki,” amesema na kueleza kuwa taasisi hizo zipo tayari kutoa mikopo kwa wajasiriamali wote wakiwemo wavuvi.